Rais Xi Jinping wa China amesema kuwa, "muungano" na Taiwan "lazima utimizwe", huku mvutano juu ya kisiwa hicho ukiendelea kutokota.

Rais wa China ameeleza kwamba, muungano huo unastahili kufikiwa kwa njia ya amani, lakini akaonya kwamba, watu wa China wana "utamaduni mtukufu" unaopinga utengano.

Ikijibu tamko hilo, serikali ya Taiwan imesema kuwa, hatima yake iko mikononi mwa watu wake. Taiwan inajichukulia kama taifa huru, huku China ikitaja kuwa mkoa wake uliojitenga.

Serikali ya Beijing imefutilia mbali uwezekano wa kutumia nguvu kufikia muungano huo. Rais Xi Jinping ameingilia suala hilo baada ya China kutuma idadi kubwa ya ndege za kijeshi katika eneo la ulinzi wa anga la Taiwan katika siku za hivi karibuni.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kuwa, hatua hiyo huenda ni onyo kwa Rais wa Taiwan kuhusu kisiwa hicho. Mwezi Mei mwaka huu, China ilitumia lugha kali zaidi katika kukabiliana  na Taiwan kwa kuonya kuwa, kisiwa hicho kujitangazia uhuru ni sawa na kutangaza vita na kwamba vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimesha jiweka tayari kuchukua hatua dhidi ya uchochezi na uingiliaji wa kigeni.

China imekuwa ikikosoa harakati za kichochezi zinazofanywa na Marekani katika langobahari la Taiwan na kueleza kwamba, kuweko manowari ya Marekani katika eneo hilo kunahatarisha amani na uthabiti katika njia hiyo ya baharini ya maji ya kimataifa.