Mkuu wa Jeshi la Myanmar amesema atawaachilia huru zaidi ya watu 5,000 waliofungwa jela kwa kushiriki maandamano ya Februari ya kupinga mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya kiraia. 

Min Aung Hlaing amesema jumla ya wafungwa 5,636 wataachiliwa mnamo mwezi Oktoba. 

Uamuzi huo umetolewa siku chache baada ya Myanmar kutengwa kwenye mkutano wa kimkoa, kutokana na serikali yake kushindwa kutuliza mzozo wa umwagaji damu unaoendelea nchini humo. 

Myanmar imekumbwa na machafuko tangu mapinduzi hayo ambapo zaidi ya raia 1,100 waliuawa na wengine 8,000 walikamatwa. Na hadi hivi sasa, zaidi ya watu 7,300 bado wako kizuizini. 

Mkuu wa jeshi hakutoa maelezo yoyote juu ya nani atakaejumuishwa katika orodha hiyo ya watakaoachiliwa, na maafisa wa gereza hawakutoa taarifa zozote kwa vyombo vya habari.