Mashamba Ya Rivacu Manyara Kumegwa Kupatiwa Wananchi
Na Munir Shemweta, WANMM MANYARA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema timu ya wataalamu itafanya tahmini kwenye mashamba mawili ya Mwada na Endamondo yanayomilikiwa na Chama cha Ushirika cha Bonde la Ufa (RIVACU) yaliyopo mkoani Manyara ili kubaini wananchi wanaotumia mashamba hayo.
Aidha, taratibu za kuondoa miliki kwenye mashamba hayo zitafanyika ili sehemu ya mashamba imegwe kwa ajili ya wananchi na sehemu inayobaki iendelee kuwa chini vyama vya ushirika.
Chama cha Ushirika cha RIVACU katika wilaya ya Babati mkoani Manyara kinamiliki mashamba manne kati ya hayo matatu yaliyoungana yapo vijiji vya Dereka Kati, Dohom na Endasago na shamba moja lipo katika kijiji cha Mwada. Shamba la Mwada lina ukubwa wa ekari 1200 na lile la Endamondo ekari 1276.
Mgogoro katika mashamba hayo unatokana na kuimarika kwa chama cha RIVACU na sehemu ya mashamba wananchi wake wamejenga makazi ya kudumu na kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Akizungumza katika ziara ya Mawaziri wa Kisekta mkoani Manyara tarehe 7 Oktoba 2021 kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 Waziri Lukuvi alisema uamuzi huo unalenga kuwapa fursa wananchi wanaofanya shughuli za kiuchumi kuendelea na shughuli zao bila ya kubughudhiwa.
‘’Katika mashamba haya taratibu za kuondoa miliki zifanyike ili sehemu ya shamba imegwe kwa ajili ya wananchi na sehemu inayobaki iendeelee kuwa chini ya chama cha ushirika cha RIVACU.
Kwa mujibu wa Lukuvi, Mpango wa matumizi bora ya ardhi utaandaliwa katika maeneo hayo ili ardhi inayotumiwa na wananchi imilikishwe kwa wahusika.
Waziri wa Ardhi ambaye ni kiongozi wa timu ya Mawaziri wa Kisekta aliwaambia viongozi wa mkoa wa Manyara kuwa, timu ya mawaziri wa inatembelea mikoa yote nchini ili kutoa mrejesho kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumnizi ya ardhi kwenye vijiji 975 na msisitizo mkubwa wa utekelezaji wake ni kutoa maamuzi yasiyoleta taharuki kwa wananchi.
‘’Rais Samia Suluhu Hassan ametuelekeza kutekeleza maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji kwa umakini mkubwa bila kuleta taharuki kwa wananchi na kwa maslahi mapana ya Taifa’’ alisema Lukuvi
Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameataka kufanyika tahmini ya fidia kwa wakazi wa Maisaka, Babati wanaoendesha shughuli zao kwenye chanzo cha maji .
Kauli hiyo inafuatia baadhi ya wananchi kugoma kuondoka eneo hilo kwa kutaka kulipwa fidia wakati baadhi yao wakiwa wameshalipwa kupisha ujenzi wa visima vya maji kwa ajili ya kusaidia mji wa Babati.
‘’Serikali inaweza kuchukua eneo lolote kwa faida ya umma au huduma za jamii na hapa mwenye chake anatakiwa kulipwa fidia na wale wananchi waliobaki wafanyiwe tathmini na kulipwa fedha zao’’ alisema Lukuvi.
Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kumtua ndoo mama kichwani kwa kusogeza huduma za maji karibu na wananchi na kubainisha kuwa, Wizara yake itamlipa mtu fidia anayesatahili na kwa suala hilo itakaa na Wizara ya Ardhi kuangalia namna ya kuwalipa fidia wananchi wliosalia.