Samirah Yusuph,
Maswa.
Mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la Ng’washi Makigo miaka 35 mkazi wa kijiji cha Mwatambuka  kata ya Lalago wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu amewauwa kwa kuwachinja na kisu wanae wawili kisha na yeye kujichinja mpaka kufa.

Tukio hilo limetokea  Octoba 22, 2021 majira saa mbili ambapo kamanda wa polisi Mkoa wa Simiyu Blasius Chatanda amewaambia waandishi wa habari kuwa mwanamke huyo alitoka na wanae kwenda kwa mdogo wake na hakumkuta kwasababu mdogo wake alikuwa ameenda zahanati kwa ajili ya matibabu.

Amesema Miili ya marehemu hao imekutwa yote ndani ya chumba kimoja nyumbani kwa Luja Makigo huku kisu kinachosadikika kutumika katika kutekeleza tukio hilo kikiwa kimebaki shingoni kwenye mwili wa mama huyo”.

“Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa mama huyo ambaye pia ni marehemu ndiye aliyetekeleza tukio hilo la mauaji (kwake na kwa watoto wake) kwa kuanza kumchinja mtoto wake mkubwa wa kike yaani Nseya Kisena na kisha kumchinja mtoto wake mdogo wa kiume yaani Majaba Kisena na hatimaye kujichinja yeye mwenyewe hadi kufa”.

Aidha ameongeza kuwa mwenyeji wa marehemu hao, Luja Makigo ambaye ni mdogo wa marehemu, alibaini tukio hilo mara baada ya kurudi nyumbani  akitokea Zahanati alipokuwa amekwenda kwa ajili ya matibabu.

Amebainisha kuwa chanzo cha tukio ni ugonjwa wa akili, kwani ndugu huyo wa marehemu wameeleza kuwa dada yake amekuwa akisumbuliwa na tatizo hilo la ugonjwa wa akili kwa muda mrefu na alishawahi kufanya jaribio la kujiua kwa kujichana shingoni kwa kutumia kiwembe miaka kadhaa iliyopita.

Aidha Kamanda Chatanda ametoa wito kwa wananchi kuongeza umakini dhidi ya watu ambao wanasumbuliwa na matatizo ya  akili, ili wasiweze kuleta madhara kwa jamii.