WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini waendelee kuiunga mkono Serikali katika mapambano ya UVIKO 19 sambamba na kuelimisha umma umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
 
Amesema hadi kufikia tarehe 22 Oktoba 2021, jumla ya wananchi 981,297 walikuwa wamechanjwa na jumla ya wagonjwa 26,154 na vifo 725 vilitolewa taarifa tangu ugonjwa huo uliporipotiwa kuingia nchini kwa mara ya kwanza tarehe 19 Machi 2020.
 
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Oktoba 27, 2021) wakati akizindua Mradi wa Mpango wa Kanisa Katoliki wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19 katika Hospitali ya Cardinal Rugambwa iliyopo Ukonga, Dar es Salaam.
 
Mradi huo unatekelezwa kupitia vituo 12 vya kutolea huduma za afya vya Kanisa Katoliki vilivyopo kwenye maeneo mbalimbali nchini ili kusaidia kujaziliza kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kudhibiti maambukizi ya UVIKO 19.

Amesema licha ya Tanzania kuudhibiti mlipuko huo, bado ugonjwa upo na wagonjwa pamoja na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vinaendelea kufuatiliwa na kutolewa taarifa huku Serikali ikitekeleza afua mbalimbali za kupambana na janga hilo pamoja na kuimarisha uchumi na huduma za jamii.
 
“Hivyo basi, tuendelee kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu kwa kujijengea utamaduni wa kuvaa barakoa safi na salama, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.”