Majaliwa: Polisi Lindi Wafikisheni Mahakamani Wezi Wa Nondo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Lindi ukamilishe upelelezi na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote wanao daiwa kuhusika katika tukio la wizi wa nondo 135 za mradi wa ujenzi wa wodi ya daraja la kwanza kwenye hospitali ya wilaya ya Nachingwea, Lindi.
“Watu wote waliohusika na wizi wa nondo za ujenzi wa mradi huu wachukuliwe hatua haraka kwani tusipoanza kuwabana watu leo, wakatambua wajibu wao wa kuwatumikia wananchi miradi mingi ya maendeleo haitakamilika.”
Mheshimiwa Majaliwa ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Oktoba 25, 2021) baada ya kukagua mradi huo wa ujenzi wa wodi ya daraja la kwanza katika hospitali ya wilaya ya Nachingwea akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Lindi.
Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mganga Mkuu wa wilaya ya Nachingwea Dkt. Charles Mtabo awe makini katika usimamizi na uendeshaji wa shughuli za sekta ya afya wilayani humo ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuhusu sekta hiyo yanafikiwa.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea Dkt. Ramadhani Maiga amesema mradi huo unaojengwa kwa awamu mbili unatekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri pamoja na mfuko wa jimbo kwa gharama ya shilingi milioni 184.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumza na madiwani, watumishi wa umma na wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Nachingwea na kuwasisitiza kila mmoja atambue kwamba yupo wilayani Nachingwea kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, hivyo atimize majukumu yake ipasavyo.
Waziri Mkuu amesema jukumu lake ni kuona kila agizo la Rais Mheshimiwa Samia linatekelezwa, ambapo amewataka watumishi hao wa umma wahakikishe uwajibikaji wao unakuwa na matokeo chanya. “Mheshimiwa Rais Samia anataka kuona kazi zenye matokeo, mkuu wa wilaya wachukulie hatua watumishi wote wasiotimiza majukumu yao.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa rai kwa Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea wasimamie vyanzo vyote vya mapato na wahakikishe fedha zote zinazokusanywa zinaingia kwenye mfuko wa halmashauri. “Ainisheni vyanzo vingine vya mapato badala ya kutegemea mazao ya korosho na ufuta tu.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia amepeleka zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye halmashauri hiyo. “Nasisitiza kwamba fedha hizi zitumike kama ilivyokusudiwa na miradi yote itekelezwe kwa viwango. Hatutakuwa na mzaha na mtumishi asiyekuwa muaminifu kwenye fedha za umma.”
Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Maafisa Mifugo nchini watenge muda wa kwenda kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu namna bora ya ufugaji ili kuondoa migogoro na uvamizi wa mifugo kwenye mashamba ya wakulima kwani hakuna sababu ya wananchi kulalamika kwenye sekta ambayo wanaisimamia.