WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametaja vipaumbele sita vya kiutekelezaji vilivyofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miezi sita tangu aingie madarakani na tayari ameonesha dira na nia thabiti katika kuwaletea maendeleo Watanzania.

Waziri Mkuu amesema katika kipindi kifupi Rais Samia ametoa fedha nyingi ambazo zimekwenda moja kwa moja katika kutekeleza miradi hiyo ikiwemo afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara, nishati na rasilimali watu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Jumanne Oktoba 26, 2021) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua na kushiriki ujenzi wa kituo kipya cha afya kinachojengwa katikati ya Vijiji vya Mvuleni na Kijiweni kwenye jimbo la Mchinga Mkoani Lindi.

Amesema Serikali ya Awamu ya sita imejikita katika kuboresha huduma za jamii na sasa malengo ya Rais Samia yanatimia kwani katika maeneo yote ya nchi miradi ya afya inatekelezwa kwa ujenzi wa zahanati katika vijiji na vituo vya afya ambavyo vinaendelea kujengwa, huku maboresho makubwa yakifanyika katika Hospitali za wilaya, mikoa na rufaa.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa katika sekta ya elimu Rais Samia amewezesha ujenzi wa madarasa katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na shule mpya ikiwa ni sehemu ya mkakati mahususi wa kuhakikisha watoto wanapata elimu bora kuanzia ngazi ya awali hadi sekondari na tayari fedha zimetolewa kwa ajili ya kuanza ujenzi.

Kwa upande wa Nishati, Mheshimiwa Majaliwa alisema Rais Samia ameendelea kutoa fedha ili kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji wa nishati ya uhakika ikienda sambamba na kuunganisha mikoa yote na umeme wa gridi ya Taifa kazi ambayo inaendelea nchini kote.

Aliongeza kuwa miradi ya maji inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ni muendelezo wa mkakati madhubuti wa Rais Samia wa kumtua mama ndoo kichwani kampeni ambayo utekelezaji wake umeanza kuzaa matunda ambapo hivi karibuni Rais alizindua mradi wa maji wa Longido Mkoani Arusha.

Aidha, Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea kuboresha sekta ya rasilimali watu na ajira akiwa amefanya maboresho ya maslahi ya watumishi na tayari kada mbalimbali za watumishi wa umma wamepandishwa vyeo na madaraja ikiendana sambamba na malipo ya malimbikizo ya madeni.

Kwa upande wake, Mbunge wa jimbo la Mchinga Salma Kikwete, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa maboresho makubwa ya miundombinu ya afya, elimu na barabara ambayo itawezesha jimbo la Mchinga kufunguka, hivyo ameiomba Serikali kumalizia ujenzi wa daraja linalounganisha kijiji Mnyangara na Mpingo ambapo alitoka mjusi wa kihistoria aliyeko Ujerumani.

Nao, wakazi wa kijiji cha Mvuleni wametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Samia kwa uamuzi wake wa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya cha kata hiyo kinachojengwa katika kijiji hicho ambacho kitawezesha upatikanaji wa huduma za afya katika eneo hilo.

“Kwa sasa tunalazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya kwani kuna kipindi akina mama na watoto walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa huduma kipindi cha kujifungua.”