Mahakama Tanzania Yaanzisha Kituo Cha Kusikiliza Masharti Ya Kifamilia
Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanzisha kituo jumuishi mahususi cha kusikiliza masharti ya kifamilia ikiwemo mirathi, ndoa, talaka, malezi na matunzo wilayani Temeke, Dar es Salaam.
Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipozindua Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki (IJCs) vya Dodoma, Arusha, Morogoro, Mwanza, Kinondoni na Temeke ambapo Tanzania inakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwa na vituo hivi.
“Hili ni jambo kubwa mno kwasababu wanawake wengi na watoto wamekuwa wakiteseka katika mambo haya,” amebainisha
Aidha, Rais Samia amepongeza uwepo wa vyumba vya kunyonyeshea watoto katika IJCs ambavyo vitawapa nafasi kina mama wenye watoto waliofika mahakamani hapo kuwanyonyesha watoto wao wakati wakisubiri huduma za haki .
Kwa upande wake, Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma amesema ujenzi wa vituo hivyo ni uwekezaji uliofanywa na Serikali katika kujenga amani, utulivu na utawala bora.
“Mihimili yote mitatu ya dola inashirikiana kwa ukaribu katika ujenzi wa Tanzania moja inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani, inayolenga kudumisha ustawi wa wananchi wa Tanzania,” amesema Prof. Juma.
Pamoja na hayo, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi ameeleza kwamba lengo la ujenzi wa IJCs ni kuboresha huduma ya utoaji haki kama inavyoelekeza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.
“Vituo hivi vitajumuisha mahakama za mwanzo, mahakama za wilaya, mahakama za hakimu mkazi, mahakama kuu, na vilevile zimejengwa sehemu kwa ajili ya majaji wa mahakama ya rufaa, lengo likiwa ni kuzifanya huduma za haki zinazotolewa na mahakama hizi zote kupatikana sehemu moja,” amefahamisha Prof. Kabudi.
Sambamba na hayo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel amebainisha kwamba mradi huo umegharimu shilingi bilioni 51 zilizotolewa na Benki ya Dunia kama mkopo wa masharti nafuu huku akifahamisha kuwa Tanzania ina mahakama za mwanzo 960, mahakama za wilaya 119, mahakama za hakimu mkazi 29, mahakama kuu 17 na mahakama ya rufani moja.
“Katika majengo hayo, tumeweka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, Ofisi ya Mawakili wa Chama cha wanasheria Tanganyika, Ofisi ya Magereza, Ofisi ya Ustawi wa Jamii na ofisi nyinginezo ili mtu anapohitaji ushauri apate kwa wepesi,” amedokeza Prof. Elisante.
Rais Samia amekuwa akiendeleza kazi ya kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya mahakama, kuongeza idadi ya majaji na mahakimu, kukuza matumizi ya TEHAMA ili kuongeza kasi ya usikilizaji wa kesi na uwekaji mzuri wa kumbukumbu sambamba na kuziimarisha taasisi nyingine za usimamiaji haki likiwemo Jeshi la Polisi.