Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, leo Jumatano Oktoba 20, 2021 inatarajiwa kutoa uamuzi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Uamuzi huo ambao utatolewa na Jaji Mustapha Siyani  unaweza kuwa picha ya mwelekeo wa kesi nyingine ndogo ndani ya hiyo kesi.

Kesi hiyo ndogo inahusiana na uhalali wa maelezo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adamu Hassan Kasekwa, ambayo mawakili wa utetezi waliyapinga yasipokewe kama kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Upande wa utetezi uliyapinga ukidai kuwa yametolewa nje ya muda wa kisheria na kwamba mshtakiwa huyo hakuyatoa kwa ridhaa yake bali kabla na wakati wa kuchukuliwa maelezo hayo alitishiwa na kuteswa.