Maelfu ya watu waliandamana jana mjini Roma nchini Italia wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wa Kundi la mataifa 20 yaliostawi na yanayoinukia kiuchumi G20 huku wakitoa wito kwao kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha upatikanaji sawa wa chanjo za ugonjwa wa COVID-19.
Waandamanaji hao ambao ni pamoja na wanafunzi na vikundi vya wafanyikazi waliandamana katikati ya jiji la Rome lililokuwa chini ya ulinzi mkali ambapo idadi ya polisi 6,000 na karibu wanajeshi 500 walipelekwa kudumisha utulivu.
Wanaharakati wa hali ya hewa waliongoza maandamano hayo, wakiwa wamebeba mabango ya rangi tofauti, kupiga ngoma na kucheza huku wakiwataka viongozi wa dunia kuokoa sayari ya dunia.
Mmoja wa waandamanaji Edoardo Mentrasti, amesema kuwa walifanya maandamano hayo kwasababu ya masuala ya kijamii na kimazingira na pia dhidi ya mataifa hayo ya G20 yanayoendelea kuchukuwa hatua ambazo zimetishia kusababisha uharibifu katika jamii na ikolojia.