Kikongwe mwenye umri wa miaka 96 na karani wa zamani wa kambi ya mateso ya Stutthof, amefika mbele ya mahakama katika mji wa kaskazini mwa Ujerumani kuanza rasmi kusikiliza mashitaka dhidi yake.
Mashitaka hayo yaliyosomwa mbele ya mahakama ya jimbo huko Itzehoe karibu na mji wa Hamburg, yanamtuhumu Irmgard Furchner kwa mauaji ya watu zaidi ya 11,000.
Mwezi uliopita, Bi Kizee huyo alijaribu kutoroka siku ya ufunguzi wa kesi yake, lakini baadaye alikamatwa na polisi na kuwekwa kizuizini.
Amefikishwa mahakamani katika kiti cha magurudumu kusikiliza kesi yake ambayo isingeweza kusikilizwa bila ya uwepo wake.
Waendesha mashitaka wanamtuhumu Furchner kwa kuwa sehemu ya mfumo wa Kinazi katika kambi ya Stutthof kufanya kazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia zaidi ya miaka 75 iliyopita.