Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza kuondolewa kwa marufuku ya nchi nzima ya kutembea usiku iliyowekwa tangu mwezi Machi mwaka 2020 kama sehemu ya juhudi za kupambana na janga la virusi vya corona. 

Akihutubia taifa katika kilele cha siku ya Mashujaa mjini Nairobi, rais Kenyatta amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kupungua kwa kisia kikubwa kiwango cha maambukizi ya Covid-19 kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki. 

Licha ya hatua hiyo, rais Kenyatta amewarai wakenya kuendelea kuheshimu kanuni zote za kiafya ili kufanikisha kurejea kwa maisha ya kawaida nchini humo. 

Kenya, taifa la watu milioni 54 limerikodi visa 252,000 vya maambukizi ya virusi vya corona na vifo vya zaidi ya watu 5,000 tangu kuzuka kwa janga hilo na hivi sasa linaendelea na kampeni kubwa ya utoaji chanjo dhidi ya maradhi hayo.