Na Munir Shemweta, WANMM KONGWA
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo amewajia juu watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma na kuwataka kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na weledi.

Mary alitoa kauli hiyo tarehe 26 Oktoba 2021 wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika ofisi ya ardhi halmashauri ya wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kufuatia kuwepo malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi kuwa kuna watumishi wa wanaodai fedha wakati wa kutoa huduma.

Alisema, wizara yake haitasita kuchukua hatia kali kwa mtumishi yeyote wa sekta ya ardhi atakayebainika kuwadai fedha wateja kinyume na gharama halisi zilizowekwa na serikali kwa kisingizio cha fedha ya usafiri.

Kwa mujibu wa Mary, ofisi yake ilipokea taarifa kutoka kwa mwananchi mmoja akidai kutakiwa kutoa kiasi cha fedha  kwa ajili ya usafiri wa kufuatilia hati jambo alilolieleza kuwa halikubaliki kwa kuwa ni kuwatesa wananchi.

‘’Tunafuatilia kwa karibu wale wote wanaodai fedha kutoka kwa wateja maana hamjawekwa hapa kuwakandamiza wananchi na suala hili halikubaliki’’ alisema Katibu Mkuu Mary Makondo.

Mary alisema, Wizara ya ardhi katika kuboresha huduma zake iko mbioni kukamilisha Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call Center) ambacho kitatumika kupokea changmoto na kero kutoka kwa wateja.

‘’Dhamana mliyopewa ninyi kama watumishi wa sekta ya ardhi ni ‘privilege’ maana ardhi inamhusu kila mtu kwa hiyo mnatakiwa kuangalia namna bora ya kutekeleza malengo ya Wizara kwa weledi’’ alisema Mary.

Akiwa katika wilaya ya Kongwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipata pia fursa ya kusalimia kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya Kongwa ambapo aliwaomba wajumbe wa Baraza hilo kushirikiana na ofisi ya ardhi kuhakikisha vijiji ndani ya wilaya hiyo vinapangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi sambamba na kuongezwa kasi ya utoaji hati za kimila.

Wilaya ya Kongwa ina jumla ya vijiji 87 na kati ya hivyo ni vijiji 41 ndivyo vyenye Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi  na kufanya vijiji 46 kusalia kupangiwa Mpango huo.

Kwa mujibu wa Mary Makondo Wizara ya Ardhi kwa sasa iko kwenye hatua za kukamilisha Miradi yake mikubwa miwili ya Benki ya Dunia pamoja na mkopo wa Benki ya Exim kwa lengo la kuhakikisha ardhi ya Tanzania inapangwa na kupimwa na kufikia malengo ya kutoa hati 2,500, 000 katika kipindi cha miaka miwili.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kongwa Job Ndugai alimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi kwa uamuzi wake wa kuitembelea wilaya hiyo kwa lengo la kutatua changamoto zilizojitokeza.

Hata hivyo, Ndugai aliweka wazi kuwa, moja ya changamoto kubwa kwenye wilaya hiyo ya Kongwa ni mashitaka yanayohusiana na migogoro ya ardhi ambapo aliiomba Wizara ya Ardhi kuangalia namna ya kuipatia wilaya hiyo Baraza la Ardhi la Wilaya ili kuwaondolea usumbufu wananchi kufuata huduma za Baraza Dodoma mjini.