Mkazi wa kijiji cha Busanda kata ya Busanda wilayani Geita Unice Kulwa(25) na wanawe wawili wamepoteza maisha baada ya kukosa hewa kutokana na kuingiza  jiko la mkaa alilokuwa akipikia maharage kwenye nyumba waliyolala.

Mbali na vifo hivyo pia baba wa familia hiyo Kulwa Kamili amenusurika kifo na amelazwa kwenye kituo cha afya Katoro akiendelea kupatiwa matibabu.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea usiku wa kuamkia Oktoba 3,2021 katika kitongoji cha Shilungule kijiji cha Busanda wilayani humo.

Aliwataja watoto waliopoteza maisha kuwa ni Kamuli Kulwa(5) na Jenipha Kulwa (3)

Credit:Mwananchi