Tangu serikali ya China ilipopiga marufuku watafiti wa masuala ya usalama kushiriki kwenye mashindano ya kimataifa kama Pwn2Own, mashindano ya Tianfu yanayofanyika kila mwaka nchini humo imekuwa sehemu kiwa wadukuzi wa China kuonesha uwezo wao

Katika mashindano yaliyofanyika Chengdu mwishoni mwa wiki, toleo jipya la iPhone ambayo inaaminika kuwa moja ya simu salama zaidi duniani, iPhone 13 Pro (yenye mfumo endeshi wa 15.0.2) lilidukuliwa mara mbili. 

Timu ya wadukuzi kutoka Kunlun Lab waliweza kuidukua simu hiyo wakati mchakato mzima ukoneshwa mbashara kwa sekunde 15. 

Hata hivyo, miezi kadhaa ya majaribio ilihusika kuwawezesha kutumia muda huo mfupi kufanya udukuzi. Taarifa kuhusu udhaifu wa simu hiyo uliowawezesha kufanikisha udukuzi hazijawekwa wazi. 

Sio Kunlun Lab pekee walioweza kudukua simu hiyo. Team Pangu waliweza kudukua simu hiyo yenye mfumo endeshe (iOS) 15. Tetesi zinadai kuwa wadukuzi hao walitumia udhaifu uliopo kwenye programu tumishi ya Safari kufanikisha hilo. 

Timu hizo zinatarajiwa kuwasilisha taarifa hizo kwa kampuni ya Apple ili iweze kuimarisha usalama wa simu zake, kwani mashindano ya udukuzi sio kosa kisheria. Katika shindano la Tianfu Cup 2021 sio bidhaa za Apple tu zilizodukuliwa, nyinginezo ni pamoja na Windows 10, Microsoft Exchange na Google Chrome.