Hukumu ya kesi ya aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na aliyekuwa makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ imekwama baada ya Aveva kushindwa kufika mahakamani.

Hukumu hiyo ilikuwa imepangwa kutolewa leo Jumatano, Oktoba 6, 2021 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kisutu, Thomas Simba.

Hata hivyo kutokana na Aveva kutokuwepo mahakamani, mahakama hiyo imeshindwa kusoma hukumu hiyo na badala yake imeiahirsha hadi Oktoba 21, mwaka huu.

Kaburu ambaye ndiye pekee aliyefika mahakamani kusikiliza hukumu hiyo ameieleza mahakama hiyo kuwa Aveva ameshindwa kufika kuwa yuko hospitalini kwa ajili ya kliniki.
Kaburu amesema kuwa Aveva anahudhuria kliniki hiyo kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.

Hakimu Simba amekubaliana na maelezo hayo ya Kaburu na akaiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 21, mwaka huu, saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya kusomwa.