Na Mathias Canal, Dodoma
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Andrea Kundo na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe Hamad Hassan Chande kwa pamoja wamekutana na kujadili kuhusu ufumbuzi wa kero ya ucheleweshwaji wa vibali (Eia Certificate) vinavyotolewa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira-NEMC.

Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Jijini Dodoma, imebainishwa kuwa kuchelewa kwa upatikanaji wa vibali hivyo kwa kiasi kikubwa imekuwa kikwazo katika miradi ya mawasiliano iliyokuwa ikihitaji Vibali kutoka NEMC.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Andrea Kundo na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe Hamad Hassan Chande katika nyakati tofauti wamewaagiza wataalamu wa Wizara hizo mbili kukaa pamoja na kuunganisha mifumo yao ili iweze kusomana na kuondoa kabisa visingizio vya kutopatikana Vibali kwa wakati.

Mhe Kundo amesema kuwa utatuzi huo wa changamoto hiyo iliyopelekea kuchelewa kukamilika kwa miradi ya serikali kwa Zaidi ya miezi saba jambo ambalo lilikuwa likirudisha nyuma utendaji na ufanisi wa kazi za serikali kwa wakati.

Amesema kuwa sasa vibali vitaanza kutoka ndani ya siku 14 mpaka 30 kutoka siku 105 za awali ambazo zilikuwa kikwazo kwa wakandarasi waliokuwa wanajenga minara mbalimbali ya mawasiliano.

“Ndugu zangu nimehangika na minara mingi ambayo imebaki viporo ikiwa na visingizio vya kutopatikana Vibali, sasa najua nani ambaye anakwamisha miradi yetu na tutachukua hatua kulingana na uhalisia” Amesisitiza Mhe Kundo

Katika kikao kazi hicho, Mhadisi Kundo amemshukuru Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe Suleiman Jaffo pamoja na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe Hamad Hassan Chande kwa kufanikisha kikao hiki ambacho kimezaa matunda.

Naibu Waziri Kundo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha Bajeti kwa ajili ya miundombinu ya Mawasiliano ambayo ni moja ya njia kuu za uchumi wa nchi.

Naye Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe Hamad Hassan Chande amesema kuwa kikao kazi hicho baina ya Wizara hizo mbili kimezaa matunda ambayo ni manufaa kwa Taifa na vizazi vijavyo kwani kimekuwa na maridhiano makubwa na muhimu.

Amesema kuwa pamoja na kuwa na makubaliano hayo yatakayopelekea maendeleo ya uwekezaji lakini ni lazima wananchi kuzingatia umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa sababu ni wazi kuwa bila mazingira hakuna maisha.

“Itakuja kuwa ni lawama kubwa sana kwa wajukuu zetu au watoto wetu kama tumewekeza kwenye maendeleo bila kujali mazingira hivyo tumekubaliana kuwa tunaenda kwenye maendeleo lakini maingira lazima tuyatazame kwa jicho la tatu” Amesisitiza Mhe Chande

Naibu Waziri Chande amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ambaye ameamua kuleta na kuwakaribisha wawekezaji na kuzifanya sera kuwa rahisi zinazowafanya wawekezaji kutokuwa na kigugumizi katika kuwekezaji nchini Tanzania.

“Ushirikiano huo unapaswa kuwa sababu ya mahusiano ya karibu ya ujenzi wa Taifa kwa pamoja kwani kufanya hivyo Taifa litafaidika na matunda ambayo yatakuwa ni endelevu wakati wote” Amekaririwa Mhe Chande

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira-NEMC Dkt Samuel Gwamaka ameahidi kufanya kazi na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini UCSAF ili kuweka mazingira mazuri ya kufanya kazi hizo.

Asema kuwa atatekeleza maelekezo yaliyotolewa na Naibu Mawaziri hao ikiwemo kutoa vibali kwa wakati kama ilivyotakiwa kutolewa ndani ya siku 14 mpaka 30.

Naye Mkuu wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote nchini Mhandisi Albert Richard amesema kuwa kikao kazi hicho kimekuwa na tija kwa kiasi kikubwa kwani serikali inadhamiria kufikisha huduma mawasiliano kwa wananchi wa mijini na vijijini ambapo hakuna mvuto wa kibiashara.

Mhandisi Richard amesema kuwa ili kufanikisha miradi hiyo ni lazima kupata vibali mbalimbali kwa wakati ikiwemo cha Mazingira ili kurahisisha na kutatua tatizo la kuchelewa kwa vibali hivyo.

MWISHO