Msemaji wa jeshi la mkoa wa Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Guillaume Njike amelituhumu Jeshi la Rwanda kuwa limevamia vijiji sita kaskazini mashariki mwa DRC Jumatatu asubuhi.

Msemaji huyo amesema, tangu Jumatatu asubuhi, jeshi la Rwanda limevamia eneo la Kibumba, mkoani Kivu Kaskazini, na kusababisha mapambano kati ya vikosi vya DRC na jeshi la Rwanda.

Ameongeza kuwa jeshi la Rwanda lililazimishwa kurudi nyuma kutokana na kupelekwa askari wa ziada wa DRC katika eneo hilo.

Wakati huo huo balozi wa Rwanda katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Vincent Karega amesema hakuna ushahidi wowote wa hujuma hiyo na kwamba askari wa Rwanda walikuwa wakimsaka mhalifu. Amedai kuwa hali ya taharuki iliyoibuliwa ni bandia. 

Hatavhiyo Jamhuri ya Kidemokarsia ya Congo imesema itawasilisha mashtaka dhidi ya Rwanda katika Jumuiya ya Kongamano la Kimataifa la Maziwa Makuu ambayo inazileta pamoja nchi za eneo hilo.

Uhusiano wa Rwanda na DRC umekuwa na panda shuka nyingi kwa miaka mingi ambapo nchi mbili hutuhumiana mara kwa mara kuhusu uvamizi au kuunga mkono waasi. Tokea Felix Tshisekedi achukue madaraka 2019 nchi hizi mbili zimeshuhudia kuboreka uhusiano na hata zimetiliana saini mapatano kadhaa kuhusu uchimbaji dhahabu.

-Parstoday