Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt Philip Isdor Mpango amekemea kuepuka siasa za makundi kabla na baada ya uchaguzi wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi  ,unaotarajiwa kufanyika 2022 ili kujenga chama imara.

Aidha amekielekeza Chama hicho ,kuanza kulitambua na kuliandaa kundi la vijana na wanawake (UWT) wenye uwezo na sifa ili kujitokeza kugombea uchaguzi huo.
 

Mpango ambae pia ni mjumbe wa kamati kuu ya CCM na mlezi wa mkoa wa Pwani, akizungumza na baadhi ya viongozi na wajumbe wa kamati za utekelezaji,aliweka mkazo kuwa makundi katika chama ni adui mkubwa na ni kansa isiyokuwa na tija .
 

Aliwaasa wanaCCM Pwani kujiepusha na siasa za makundi ili kujenga na kuimarisha chama hicho na kujenga upendo .
 

“Tukatafute suluhu kwenye vikao na ikiwezekana kutumia wazee Kupata busara zao ,na hata Mimi niiteni nitakuja Kama mlezi ili tuyamalize wenyewe ndani “alifafanua Mpango.
 

Hata hivyo Mpango alisema maandalizi ya uchaguzi huo ni muhimu kufanyika mapema ili kujua nguvu iliyopo .
 

“Nasikia mna Jambo lenu 2025 ,sasa ni wakati wenu kuanza kujiandaa na uchaguzi huu ndani ya chama ili mkifikia mwaka huo muende sawa”alieleza Mpango.
 

AMANI
Mpango katika hili anasisitiza kulinda amani na utulivu ambapo ni tunu ya Taifa na Kila mtanzania ana wajibu wa kulinda amani na usalama.
 

“Tushirikiane kufichua wale ambao tunawashuku wanataka kuharibu amani yetu ,”
 

UHAI WA CHAMA
Mlezi huyo wa CCM Pwani, aliwataka viongozi wa CCM mkoa wa Pwani kuhakikisha wanakuwa na mtaji wa kutosha wa wanachama walio kwiva kiitikadi .
 

“Sio leo mtu anaingia kesho kageuka ,kubwa zaidi kutafuta wanachama ,tusiridhike kwani uchaguzi ni namba “
 

Pia Mpango alisisitiza ,ulipaji ada na kuwaasa viongozi hao kuhamasisha kulipa ada ,hili ni takwa la kikatiba
 

VIKAO
Katika hili ,Mpango alisema chama ambacho hakifanyi vikao maendeleo yake ni hafifu hivyo izingatiwe kalenda ya vikao ili kushauriana masuala mbalimbali .
 

Alitaka ziara za kukagua uhai wa chama zifanyike kwa Jumuiya zote za chama, anaeleza kura zipo pembezoni ikiwemo mkoani Pwani lazima kufika maeneo hayo kukagua uhai wa chama.
 

Makamu huyo wa Rais ,aliwataka wabunge,wabunge wa viti maalum na madiwani kwenda kuongea na wananchi ,kujua kero zao na kuzitafutia ufumbuzi zile zilizo ndani ya uwezo wao .
 

Alitaka ratiba za mikutano watakayoifanya iwepo nakala kamati za siasa za chama .
 

Mpango alihimiza umuhimu wa semina na kuwataka wanachama kujisajili kwenye mfumo wa kielektroniki.
 

MIRADI YA KIMAENDELEO NA KIUCHUMI
Mpango alisema ,kila kiongozi na wanaCCM kusimamia miradi ya mendeleo kujua maendeleo ya miradi hii na kusimamia watendaji wa serikali maeneo yanayogusa wanyonge wakiwemo wazee.
 

Alielekeza kujiimarisha kiuchumi na kuibua miradi ili kujiongezea mapato .
 

“Siasa nzuri na bora zinaendana na uchumi wa uhakika ,naomba CCM na Jumuiya kusimamia miradi ya sasa pia iwe endelevu na mchunge wale wanaotumia miradi ya Chama kujinufaisha “
 

Alielezea,kukiwa na miradi ya uhakika kutaondoa hali ya kuwa ombaomba na vijana kutonunulika kirahisi.
 

Akizungumzia kuhusu chanjo ya Uviko 19, Mpango amewaasa viongozi wa chama,kuchukua dhamana ya kuhamasisha chanjo hiyo ili watu wajilinde na ugonjwa huo .
 

Ugonjwa huu upo ,”Mimi mwenyewe niliugua ugonjwa huu najua adha yake “viongozi wa chama tuhamasishe hili kuanzia ngazi ya chini ,tuchukue hatua huku tukizingatia maelekezo ya watalaamu wetu wa afya”anasisitiza Mpango.
 

Nae mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini ,Silvestry Koka ,alisema anajivunia kuona ushirikiano mkubwa uliopo baina ya CCM Pwani na Serikali mkoa.
 

Koka alisema , maelekezo yatazingatiwa na kusema hakuna shaka kwani mahusiano yanaimarishwa .
 

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani ,Ramadhani Maneno alisema aliyoyasema mlezi huyo wameyabeba na kwenda kuyafanyia kazi.