Na.WAMJW-St.Petersburg,Urusi
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Afya wa Urusi Mhe. Viktor Sergeevich Fisenko.

Katika mazungumzo yao mawaziri hao wamejadili mambo mbalimbali  yakiwemo ya ushirikiano katika sekta ya Afya na Maendeleo ya Jamii baina ya nchi hizo mbili.

Dkt. Gwajima amesema kutokana na mashirkiano ya takribani miaka 60 sasa nchi hizo zitaendeleza ushirikiano katika maeneo ya miundombinu ya Afya, Makao ya watoto yatima, nyumba za wazee, uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha dawa za binadamu ,mafunzo kwa madakatari bingwa na  bobezi, kubadilishana wataalam na uzoefu, tiba mbadala pamoja na huduma za telemedicine.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema kwamba wapo tayari kuandaa rasimu ya Mkataba wa  Ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Urusi katika masuala ya Afya na maeneo mengine muhimu katika sekta ya Afya.

Dkt.Gwajima amefafanua kwamba Tanzania inaelekea Kwenye matibabu ya kitalii hivyo nchi inahitaji wataalam wenye uwezo kwenye eneo hilo hivyo Kwa kutumia huduma za telemedicine kwani Warusi wapo juu sana kwenye huduma hivyo vilevile wao wanaweza kuwekeza huduma zao kupitia Bodi ya Usajili ya vituo binafsi na hivyo itaongeza ajenda ya nchi ya kutangaza matibabu ya kitalii.

Kwa upande wa bima ya afya kwa wote Waziri Dkt. Gwajima amesema wanapokuja watalii wataweza kukata Bima hiyo na kuweza kupata huduma kwani Tanzania na miundombinu na uwezo wa kuwatibu kwa  vifaa  vilivyopo sio mdogo.

Naye Naibu Waziri wa Afya wa Shirikisho la Urusi Mhe. Viktor Sergeevich Fisenko   amesema wanayo furaha kushirikiana na nchi ya Tanzania na kwamba ushirikiano baina ya nchi hizo mbili una faida kwa pande zote hivyo nchi ya Urusi wapo tayari kushirikiana katika maeneo yaliyobainishwa ikiwemo viwanda vya madawa ,mafunzo na kubadilishana uzoefu.

Aidha, amesema anayo furaha kuona maambukizi ya UVIKO-19 nchini Tanzania yanapungua na njia zote zinatumika  kukabiliana na ugonjwa huo zimekuwa na manufaa na hivyo Urusi ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika mbinu ambayo nchi yao imekua inakabiliana nayo ikiwemo chanjo na kuhakikisha mashirikiano yaliyokuwepo baina ya  nchi  hizi mbili yanaendelea.

Naibu Waziri huyo amesema zoezi la kutoa chanjo ya UVIKO-19 kwa nchi ya Urusi linaendelea vizuri na  zaidi ya watu  milioni 50 wameshapata dozi ya kwanza, na watu milioni 48 wameshapata dozi mbili na pia watu milioni mbili wameshafanya marudio chanjo ( _revaccination_ )  dhidi ya UVIKO-19. Chanjo zinazotumilka nchini Urusi ni    _Sputnik-V_ na  _Sputnik  Light_.