Samirah Yusuph,

Busega.
Wanafunzi 13,933 wa shule za sekondari wilayani Busega Mkoa wa Simiyu wanakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa hali ilinayoweza kushusha kiwango cha elimu wilayani hapo.

Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya hiyo  Gabriel Zakaria wakati wa hafla ya kuchangia ujenzi wa wa vyumba vya madarasa iliyofaanyika usiku wa Octoba 2, 2021.

Amesema kuna upungufu wa vyumba vya madarasa 79 viti na meza 3950 vyenye thamani ya tsh752 milioni huku matarajio ya wanafunzi watakao jiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 ni 6442 na kufikisha idadi ya wanafunzi  20,375.

"Kwa idadi hii ya wanafunzi vyumba vilivyopo havijitoshelezi kuwahudumia wote hivyo hatua ya dharura ni lazima zichukuliwe ili kuhakikisha wote wanapata nafasi ya kwenda shule" amesema Gabriel.

Ameongeza kuwa katika hatua za awali madarasa yanayo jengwa na yamefikia hatua mbali mbali yapo 76 huku mahitaji ya vifaa vya ujenzi ili kukamilisha bado ni mkubwa.

Wakizungumza baada ya hafla hiyo wadau wa elimu waliohudhuria katika hafla hiyo wamesema kuwa ubora wa elimu unaendana na ubora wa miundombinu hivyo ni jukumu la kila mmoja kuboresha mazingira ya mtoto kupata elimu.

"Serikali inamchango wake katika kuinua ubora wa elimu na wadau wanamchango wao pia ili kuunga mkono juhudi binafsi zinazofanywa na viongozi wa serikali ambao wamewiwa kuhakikisha watoto wanapata elimu bora" amesema Dr Raphael Chegeni mdau wa maendeleo wilayani Busega.

Aidha mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Busega Sundi Mniwe Amesema kuwa bado wanaendelea kukusanya na kupokea michango mbali mbali ili kumaliza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa.

"Tuna wanafunzi wengi, na ni ukweli ambao haufichiki kuwa baadhi ya kata bado zina shule zenye majengo yasiyojitosheleza hivyo zinalemewa tumelazimika kuanzisha michango ili kuwezesha baadhi ya kata ziwe na shule mbili za sekondari".

Katika hafla hiyo wamefanikiwa kupata kiasi cha  tsh82 milioni pamoja na seruji mifuko 2,286.

Mwisho.