Na Dotto  Kwilasa/CCM Blog
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha majadiliano yaliyopelekea kupata fedha za msaada na mkopo wa masharti nafuu kutoka shirika la fedha la kimataifa (IMF) na kusema Kuwa hatua hiyo imedhihirisha upeo na uwezo alionao katika kutetea na kulinda maslahi ya watanzania.

Hatua hii imekuja kufuatia  hatua ya hivi karibuni Rais  Samia  kuzindua kampeni kubwa ya Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVICO-19 ambayo inagharimu takribani trilioni 1.3 fedha zitakazoleta unafuu katika mapambano ya Ugonjwa huo.

Hayo yamesemwa jana  Jijini Dodoma na Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM-Taifa,Itikadi na uenezi Shaka Hamdu Shaka katika mkutano wake na Waandishi wa habari huku akieleza kuwa hatua hiyo ni Utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa chama hicho ya mwaka 2020 hadi 2025.

"Niwakumbushe watanzania,CCM ndiyo imeshika hatamu za uongozi wa Nchi hivyo tunawahakikishia kuwa fedha hizi hazitafunwi na mchwa watu,atakayethibitika kuhusika na ukwapuzi wa aina yoyote Chama hakitasita kuielekeza Serikali kutumia sheria,"amesema Shaka.

Kutokana na hayo,Katibu huyo mwenezi amezielekeza Wizara zote zitakazonufaika na fedha hizo kujipanga vizuri katika usimamizi kama alivyoelekeza Mama Samia na kusisitiza kuwa Viongozi Wenye dhamana kuanzia Serikali kuu hadi kwenye Halmashauri za Wilaya kuhakikisha fedha hizo zinatekeleza miradi iliyokusudiwa na kuleta matokeo chanya.

Wakati huo huo chama hicho pia kimekupongeza Chama Cha ACT-Wazalendo Kwa ushindi katika Jimbo la Konde,Wilaya ya Micheweni,Mkoa wa Kaskazini Pemba na kusema kuwa hatua hiyo imefikiwa ili kuwaonesha watanzania kuwa CCM inaendeshwa kwa maana halisi ya dhana ya siasa safi na demokrasia ya kweli.

"Tunawashukuru wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Konde kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi ijapokuwa kura hazikutosha,tunaamini maneno ya wahenga kuvunjika kwa koleo  sio mwisho wa uhunzi na tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kweli katika Maendeleo ya Jimbo hilo,"ameeleza.

Licha ya hayo Shaka amesema  kumalizika kwa uchaguzi huo mdogo kwa amani na utulivu ni jambo la kujivunia Kwani jamii itaendelea kujifunza na kuuishi umoja na ushirikiano  na hatimaye kuleta maendeleo ya kiuchumi.

"Tunawapongeza na kuwashukuru Kwa dhati Wananchi wote wa Jimbo la Ushetu,Mkoa wa Shinyanga Kwa kumchagua Emanuel Peter Kwa kura za kishindo,tunawashukuru pia watanzania kwa kuendelea kutuamini hususani kwa ushindi waliotupatia katika kata tatu za Neruma-Bunda(Mara),Lyowa-Kalambo(Katavi) na vumilia-Urambo(Tabora)."