Mahakama  ya Hakimu Mkazi Arusha imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake baada ya kukutwa na hatia ya unyang’anyi kwa kutumia silaha.

Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Arusha, Odira Amworo amesema kuwa ameridhika mashtaka dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake na kuwatia hatiani kosa unyang’anyi wa kutumia silaha.

Baada ya kuwatia hatiani wakili wa Serikali amesema hakuna kumbukumbu ya makosa ya zamani ya washtakiwa wote watatu, na kuiomba Mahakama iwape adhabu ya miaka isiyopungiua 30 jela na viboko.

Hukumu yakesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha iliyokuwa ikimkabili Sabayahiyo imesomwa leo Ijumaa Oktoba 15, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo.

Kabla ya kuanza kusomwa hukumu, Wakili wa Serikali, Felix Kwetukia aliweka wazi kuwa Jamhuri ipo tayari kupokea hukumu huku upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Moses Mahuna, Silvester Kahunduka na Wakili Fridolin Germelo nao walisema wapo tayari kusikiliza hukumu hiyo.

Hakimu Omworo amesema kuwa imethibitika mshitakiwa wa kwanza alikuwa na bastola ndani na nje kulikuwa na watu wawili wenye silaha hivyo, hakuna shaka duka la shahidi wa kwanza lilivamiwa na watu wenye silaha na lilikuwa chini ya watu wenye silaha.

Washtakiwa, Sabaya na wenzake walifikishwa mahakamani leo saa 3:05 asubuhi, kwa ajili ya hukumu ambapo Oktoba 1 2021 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Amalia Mushi aliahirisha hukumu hiyo kwa maelezo ya kutokamilisha kuandika hukumu hiyo.