Tunapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa zisizo sahihi za upangaji wa mikopo wa wanafunzi wa elimu ya juu ambazo zimekuwa zikisambazwa mitandaoni kuanzia jana, Oktoba 23, 2021.

Ufafanuzi wa jumla:

Hakuna mwanafunzi aliyepangiwa mkopo wa TZS 2,750 kwa mwaka wa masomo 2021/2022. Kati ya wanafunzi 45,095 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mkopo hadi sasa, mwanafunzi mwenye kiwango cha chini cha mkopo ni TZS 2,099,500 na kiwango cha juu ni TZS 6,431,500;

👉Kutazama majina ya Waliopata Mkopo awamu ya kwanza na ya  pili  <<BOFYA HAPA>>

 Upangaji mikopo huzingatia uhitaji wa wanafunzi na kipaumbele hutolewa kwa waombaji yatima, wenye ulemavu, waliofadhiliwa katika elimu ya sekondari na wanaotoka katika kaya masikini ambao wameomba mkopo kwa usahihi na kupata udahili;

Viwango vya jumla (lumpsum allocations) vya mikopo kwa wanufaika huzingatia uhitaji wa mwombaji na mahitaji ya kozi ya mnufaika mmoja mmoja. Mnufaika anaweza kupangiwa kipengele kimoja au zaidi kati ya (i) Chakula na Malazi, (ii) Ada ya Mafunzo, (iii) Mafunzo kwa Vitendo, (iv) Mahitaji Maalum ya Vitivo (v) Vitabu na Viandikwa, na (vi) Utafiti. Hivyo, mnufaika hupangiwa vipengele kulingana na uhitaji wake na ambavyo vimo katika kozi aliyodahiliwa;

Kuhusu malipo ya fedha za chakula na malazi (Meals and Accommodation), kwa sasa, kila mnufaika hulipwa ni TZS 8,500 kwa siku na hulipwa kwa mikupuo minne kwa mwaka wa masomo na kwa wastani kwa kila mkupuo ni TZS 510,000;

Kuhusu idadi ya wanufaika wa mwaka wa kwanza, mpaka sasa jumla ya wanufaika wapya wapatao 45,095 wamepangiwa mikopo katika awamu mbili na awamu ya tatu inayotarajiwa kutolewa Oktoba 25, 2021 itakuwa na wanufaika wapya wasiopungua 12,000;

👉Kutazama majina ya Waliopata Mkopo awamu ya kwanza na ya  pili  <<BOFYA HAPA>>

 Aidha, kwa wanafunzi ambao hawajaridhika na kiwango walichopangiwa sasa, dirisha la rufaa litafunguliwa mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2021. Dirisha hili ni fursa kwa wanafunzi kuwasilisha maombi ya kuongezewa viwango vya mikopo.

Hitimisho

Tunatoa wito kwa wanafunzi-wanufaika wa mikopo kuendelea kufuatilia taarifa za mikopo kupitia akaunti zao mahususi zinazojulikana kama SIPA.  

Aidha, kwa wanafunzi waliopo vyuoni, wawasiliane na Maafisa Mikopo ili kufahamu ratiba za maafisa wa HESLB watakaofika vyuoni kukutana na wanafunzi na kufafanua masuala mbalimbali yanayohusu mikopo.

Imetolewa na:

Abdul-Razaq Badru,

MKURUGENZI MTENDAJI 

👉Kutazama majina ya Waliopata Mkopo awamu ya kwanza na ya  pili  <<BOFYA HAPA>>