Na Steven Nyamiti-WM
Waziri wa Madini,  Doto Biteko ameiagiza Tume ya Madini kuanza kutoa vibali vyote vya madini kwa wafanyabiashara wa madini katika eneo la Mahenge Ulanga ili kuondoa usumbufu wa kusafiri umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 300 hadi mkoani Morogoro kwa ajili ya kufunga mizigo yao.

Ameelekeza agizo hilo lianze kutekelezwa Novemba Mosi, 2021 ili wafanyabiashara wa madini wapate huduma zote muhimu kuanzia kufanyiwa uthaminishaji, upimaji, ukataji, ufungaji na uongezwaji wa thamani ili manufaa hayo yabaki kwa wananchi wa Ulanga.

Waziri Biteko ametoa agizo hilo  Oktoba 22, 2021 wakati akifungua Tamasha la Kuhamasisha Fursa za Uwekezaji linalofanyika katika Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.

Aidha, Waziri. Biteko amesema, mchakato wa kuanzisha Mkoa wa Kimadini wa Mahenge Ulanga unaendelea ili kurahisisha shughuli za uchimbaji wa madini kwa wanachi wa Mahenge kwa kuwasogezea huduma karibu.

Akizungumzia umuhimu wa Sekta ya Madini, Waziri Biteko amesema kuwa,uwepo wa shughuli za madini zina mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa, hususan katika utoaji wa ajira na mapato yatokanayo na shughuli hizo.

“Uwepo wa shughuli za madini zina mchango mkubwa sana kwa maeendeleo ya Taifa, hasa katika utoaji wa ajira na mapato yatokanayo na shughuli hizo,”amesema Waziri Biteko.

katika kuhamasisha Fursa za Uwekezaji, Waziri Biteko amepongeza uongozi wa Wilaya ya Ulanga kwa kuanzisha na kufanikisha Tamasha la Kuhamasisha Fursa la Uwekezaji kwa kushirikiana na wadau wengine.

Amesema, kupitia tamasha hilo, kutachochea uwekezaji katika Wilaya ya Ulanga kwa kwa kuleta maendeleo ya kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Bi. Ngollo Malenya amesema, Wilaya ya Ulanga ina fursa za uwekezaji katika uchimbaji wa madini, ubia na wamiliki wa leseni za maeneo ya madini ambao wana leseni lakini hawana mitaji, vifaa na teknolojia ya uchimbaji wa madini.

“Kuna fursa ya kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa vya kukata na kuchakata madini, kutoa huduma katika migodi, mikopo kwa wachimbaji wakubwa na wadogo na kunufaika na Soko la Madini la Ulanga,”amesisitiza Malenya.

Aidha, ameeleza madini yanayopatikana katika Wilaya ya Ulanga ni pamoja na madini ya Kinywe (graphite) ambapo madini hayo yamekuwa yakihitajika sana duniani katika utengenezaji wa betri, madini ya Spinel, Rubi na Dhahabu.

Tamasha la Kuhamasisha Fursa za Uwekezaji linalofanyika katika Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro linakwenda na Kauli Mbiu isemayo  “Amazing Ulanga” kauli mbiu inayoashiria uhalisia wa Wilaya ya Ulanga.

Aidha, tamasha hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wakuu wa wilaya na wadau mbalimbali wa sekta nyingine ili kujadili kwa pamoja fursa za maendeleo zinazopatikana katika Wilaya ya Ulanga.