Sekretari wa zamani kwenye kambi ya mateso ya Wanazi aliyejaribu kukimbia kabla ya kesi yake kuanza, ameachiliwa kutoka kizuizini kuelekea kusikilizwa tena kwa kesi hiyo. 

Irmgrad Furcher mwenye umri wa miaka 96 alikuwa apandishwe kizimbani Alkhamis iliyopita, kukabiliana na kesi ya kushiriki mauaji ya watu zaidi ya 10,000 katika kambi ya mateso ya Stufhof nchini Poland, lakini badala yake akashindwa kuhudhuria mahakamani akijaribu kukimbia.

Bibi huyo alikamatwa na polisi masaa kadhaa baadaye, na tangu hapo aliwekwa kizuizini akisuburi kesi yake kutajwa tena tarehe 19 mwezi huu. Hata hivyo, mahakama katika mji wa kaskazini wa Itzehoe imeamuwa kuwa bibi huyo anaweza kuachiliwa kwa masharti maalum. 

Akiwa mmoja kati ya wanawake wa kwanza kushitakiwa kwa uhalifu wa zama za Wanazi, Bi Furchner anatuhumiwa kusaidia mauaji ya mahabusu wakati akifanya kazi kwenye ofisi ya kamanda wa kambi hiyo, Paul Werner Hoppe, baina ya Juni 1943 na Aprili 1945.