SALVATORY NTANDU
Mkazi wa Mtaa wa Mbulu Kata ya Mhongolo Halmashauri ya Manispaa ya Kahama Regina Jiyenze (45) ameuawa na mume wake aliyejulikana kwa jina la Heneriko John (53) kwa kumkata na panga katika sehemu mbalimbali za mwili akimtuhumu sio mwaminifu katika ndoa yao na  kisha kujisalimisha katika kituo cha polisi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga (ACP) George Kyando amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo yaliyotokea  Oktoba tano mwaka huu majira ya saa tatu asubuhi nyumbani kwa balozi wa nyumba 10 aliyejulikana kwa jina la Manungu Bundala.

“Chanzo cha mauaji hayo ni  wivu wa kimapenzi ambapo mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu mkewe kuwa sio mwaminifu kwenye ndoa yao, hali iliyosababisha kujichukulia sheria mkononi kwa  kumkata panga kichwani na mabegani na kumsababishia kupoteza Maisha,”alisema Kyando

Amesema kuwa eneo la tukio liliokotwa  panga lenye damu lililotumika kutekeleza mauaji hayo, na mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi mara baada ya kujisalimisha mwenyewe, katika kituo cha polisi kahama na tutamfikisha mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

“Mbinu iliyotumika kutekeleza mauaji hayo ni mtuhumiwa  kumvizia marehemu wakati akiwa nyumbani kwa balozi Manungu Bundala, alipofika kwa ajili ya kushtaki kutishiwa kuuawa na mume wake, ndipo alipokatwa mapanga sehemu za kichwani na mabengani na kufariki dunia,”alisema Kyando.

Sambamba na hilo kamanda  Kyando ametoa wito kwa wanandoa  kuacha kujichukulia sheria  sheria mkononi, pindi wanapotofautiana kauli hususani wanapotuhumiana kuhusiana na masuala ya mapenzi na badala yake waende dawati la jinsia,ustawi wa jamii,viongozi wa dini na wasipofikia muafaka  ni bora wakaachana.

Mwisho.