Askofu wa Kanisa la Uamsho la Moravian, Emmaus Mwamakula, ameendesha maombi maalum katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kabla kesi inayomkabili kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake kuanza.

Askofu Mwamakula ameendesha maombi hayo leo Jumatano, tarehe 20 Oktoba 2021, kabla ya mahakama hiyo haijaanza kutoa uamuzi dhidi ya kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi ya msingi ya uhujumu uchumi, Adam Kasekwa, yasitumike mahakamani hapo kama sehemu ya ushahidi wa jamhuri.

Akiwaongoza mawakili wa utetezi, Askofu Mwamakula amemuomba Mungu aingilie kati kesi hiyo, ili haki itendeke. Wakati wa maombi hayo, mawakili hao na watu wengine walisimama wakati maombi yakiendelea.

Mahakama hiyo mbele ya Jaji Kiongozi Mustapha Siyani, ilipanga kutoa uamuzi wa kesi hiyo ndogo jana tarehe 19 Oktoba 2021, lakini ilishindikana kutokana na kuwa siku kuu ya maulid, hivyo imepanga kutoa leo.