Mtu anayedaiwa kuwa ni mlinzi wa Kampuni ya Suma JKT, Emmanuel Myela (35) mkazi wa Wilaya ya Mbozi, amelazwa katika hospitali teule ya rufaa mkoani Songwe baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira, alipokuwa akivizia watu wanaosafirisha bidhaa za magendo toka nchi jirani ya Malawi Oktoba 17.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Janeth Magomi alipoulizwa kwa simu kuhusu tukio hilo amesema kwa sasa hawezi kulizungumzia kwa kuwa hakuwa na taarifa iliyo kamili.

Mmoja wa shuhuda aliyekuwepo eneo la tukio, Mussa Mgode amedai kwamba askari hao ambao walikuwa watatu hawakuvalia sare za jeshi wakiwa na pikipiki mbili walifika eneo hilo majira ya saa 9 alasiri kisha walimkamata mtu mmoja waliyedai kuwa amebeba magendo hayo.

Alisema baada ya kumkamata mtu huyo palitokea mabishano kati yao na ndipo walipojitokeza wenzao kadhaa ambao waliamua kupambana na ‘askari hao’.

Kama hiyo haitoshi, shuhuda huyo alisema lilijitokeza kundi la wananchi waliokuwa wakitokea kwenye msiba na kuanza kuwasaidia vijana hao na ndipo askari wawili walifanikiwa kukimbia kusikojulikana wakizitelekeza pikipiki zao mbili ambazo baadaye zilichomwa moto na wakazi hao.

Hata hivyo, mmoja wao aliyebaki alikimbilia nyumba iliyo jirani na kujifungia, lakini wananchi kwa hasira walivunja dirisha la nyumba hiyo na kumtoa nje na kuanza kumshushia kipigo kikali kabla ya Polisi kufika na kumuokoa.

Kaimu Mganga Mfawidhi, Dk Lighton Alex amethibitisha kumpokea majeruhi huyo akiwa hajitambui kutokana na kipigo.

Amesema askari huyo alifikishwa katika Hospitali hiyo kwa gari ya polisi baada ya kuokolewa kwenye kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira kali.

Amesema baada kumfanyia vipimo vya mionzi ilibainika kuwa majeruhi huyo alipata mpasuko kwenye fuvu lake la kichwa.

Credit:Mwananchi