Kiongozi wa upinzani nchini Urusi aliye gerezani ambaye pia ni mkosoaji mkubwa wa rais Vladmir Putin, Alexei Navalny ametunukiwa tuzo ya juu kabisa inayotolewa na Umoja wa Ulaya kuhusu haki za binadamu. 

Katika ishara ya wazi ya ukosoaji kwa Ikulu ya Kremlin, viongozi wa bunge la Umoja wa Ulaya wamemteua Navalny kupokea tuzo hiyo kutoka kundi lililojumuisha wagombea wengine ikiwemo rais wa zamani mpito nchini Bolivia Jeanine Anez. 

Tangazo kuhusu tuzo hiyo limetolewa kupitia ukurasa wa Twitter wa Bunge la Ulaya likiwa pia na ujumbe wa kuzitaka mamlaka nchini Urusi kumuachia huru kiongozi huyo wa upinzani aliyekamatwa na kutupwa gerezani mwazoni mwa mwaka huu. 

Uamuzi wa kumtunuku tuzo hiyo Navalny yumkini utadhoofisha zaidi mahusiano yaliyopwaya kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi tangu Moscow ilipoinyakua kwa nguvu rasi ya Crimea mwaka 2014 na ilipotuhumiwa kuhusika na shambulizi la sumu dhidi ya Navalny.