Wizara Ya Afya Yakabidhi Magari Kwa Ajili Ya Ufuatiliaji Afya Mazingira Na Usafi Dodoma
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, amekabidhi magari kwa ajili ya ufuatiliaji wa shughuli za afya mazingira na usafi kwenye Mikoa sita nchini huku akiagiza yatumike kwa malengo yaliyokusudiwa.
Dk.Gwajima ameyasema hayo jana jijini Dodoma alipokuwa akikabidhi magari hayo kwenye mikoa ya Kagera, Mara, Manyara, Tabora, Songwe na Mtwara ambayo yamenunuliwa kupitia mfumo wa Lipa kwa matokeo.
Amesema kuna magari yanayotolewa kwa ajili ya program za afya ambapo yamekuwa yakitumika kwa shughuli zingine huku shughuli husika yakitumika kwa asilimia 25.
“Tunaanza sensa ya kwa kiwango gani magari yanayopelekwa kusimamia program za afya yanatumikaje huko yanakokwenda, hatusemi sekta ya afya isiwe ushirikiano na sekta nyingine tunataka uwiano katika matumizi ya magari hayo na kazi gani linafanya kazi kusaidia sekta nyingine maana zote ni sekta za serikali,”amesema.
Amefafanua kuwa Wizara inatekeleza program ya huduma endelevu za maji na usafi wa mazingira yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa maji na huduma za usafi wa mazingira vijijini ambayo inatekelezwa mikoa 17 katika Halmashauri 86 nchini.
Amebainisha sababu ya kuchagua mikoa hiyo ni kwa kuzingatia vigezo vya hali duni ya upatikanaji wa huduna za maji na usafi wa mazingira, kiwango cha umasikini na kiwango cha juu cha udumavu wa watoto.
Amesema na kupitia programu hiyo mikoa na halmashauri zimeendelea kuboresha huduma za maji na usafi wa mazingira kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na jamii na kwa mwaka wa fedha 2020/21 halmashauri zimetekeleza katika vituo vya kutolea huduma za afya 873 nchini.
Aidha, Dk.Gwajima amesema serikali imenunua pikipiki 138 ambazo tayari zinatumia na maafisa afya ngazi ya kata kama sehemu na utatuzi wa tatizo la usafiri na yatanunuliwa magari mengine matano.
Awali, akizungumza niaba ya kwa Mkurugenzi wa Kinga wa Wizara hiyo, Dk.Leonard Subi, Mratibu wa Kampeni ya Usafi wa Mazingira, Anyitike Mwakitalima, amesema magari hayo yamegharimu zaidi ya milioni 646.