WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapa muda wa mwezi mmoja viongozi wa mikoa na halmashauri wawe wamekutana na wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga na kupanga namna bora ya usimamizi wa shughuli za biashara ikiwemo kutenga maeneo ya kufanyia biashara zao.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa jana wakati akizindua mpango wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi wa 2022, ambapo aliwataka Wakuu wa Mikoa wawe makini katika zoezi la kuwapanga Wamachinga nchini na kuepuka vurugu, fujo na uonevu.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Septemba 15, 2021) wakati akizungumza kwa njia ya video na Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Waziri wa Viwanda na Biashara, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Uongozi wa Wamachinga.

Waziri Mkuu amewaelekeza viongozi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa, Miji na wilaya  waone namna ya kutumia baadhi ya barabara za katikati ya majiji na miji kufungwa muda wa alasiri ili kuruhusu Wamachinga kufanya biashara zao katika barabara hizo.. “Hii ni fursa nzuri kwa wajasiriamali wetu kufanya shughuli zao.”

Amesema viongozi hao wa mikoa kwa kushirikiana na viongozi wa machinga na machinga wanaweza kutenga maeneo maalumu na kuanzisha magulio ya mwishoni mwa wiki, utaratibu huo utawezesha wajasiriamali wengine kufanya shughuli zao za kiuchumi kama madereva wa bodaboda, machinga na taksi watakaokuwa wakisafirisha abiria.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wahakikishe maeneo watakayoyatenga kwa ajili ya wamachinga kufanya biashara zao yanatambulika na yanakuwa na miundombinu muhimu kama vyoo, maji ili kuyaboresha.

 Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara ina mkakati wa kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo kwa lengo la kuwapa uelewa mpana wa  biashara wanazofanya.

Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Ummy Mwalimu amesema wamepokea maelekezo hayo na kwamba tayari wameshaanza kuandaa muongozo wa kuratibu shughuli za Wamachinga ambao utawawezesha viongozi wa mikoa kuweza kuwasimamia wafanyabiashara hao.

Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara ametumia fursa hiyo kuwahakikishia Wamachinga pamoja na wafanyabiashara wadogo nchi kwamba kwa sasa rasmi Serikali katika sera ya Biashara Ndogo ndogo (SME) nchini imewatambua Wamachinga.

Awali, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamachinga Tanzania, Ernest Matondo Masanja pamoja na mambo mengine ameishukuru Serikali kwa hatua inazochukua kuhusu Machinga na kwamba ameahidi kuendelea kushirikiana nayo.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU