WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi katika eneo la Ngangamfumuni, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema mradi huo ni wa kimkakati kwani mkoa wa Kilimanjaro upo mpakani hivyo uwepo wa kituo cha mabasi cha kisasa utatoa fursa kwa wakazi wa mkoa huo kufanya biashara kwa kuwa utapokea mabasi kutoka nchi za jirani ikiwemo Kenya.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 23, 2021) wakati akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Manispaa Moshi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kituo hicho akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa serikali katika mkoa huo.

“Hiki ni kituo cha mabasi chenye hadhi ya kimataifa, mkoa huu unapokea watalii wengi kutoka katika maeneo mbalimbali, hivyo ujenzi wa hoteli katika kituo hiki utasaidia kuongeza fursa za biashara kwa wakazi wa hapa”

Naye, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashidi Gembe amesema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 28.86 unatekelezwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa jengo la abiria lenye ukubwa wa mita 13,979 ikijumuisha sakafu ya chini ya ardhi na ghorofa mbili kwa gharama ya shilingi bilioni 17.9.

“Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa jengo la hoteli lenye ghorofa nne kwa gharama ya shilingi bilioni 11.40. Mradi huu utakapokamilika unatarajiwa kuiongezea Halmashauri wastani wa mapato ya shilingi bilioni 2.72 kwa mwaka kutokana na makusanyo ya ushuru na kodi zitakazokusanywa.”

Baada ya kuweka jiwe la msingi katika kituo hicho, Mheshimiwa Majaliwa alikagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Tella Mande uliopo Moshi vijijini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wa kufikisha huduma ya maji vijijini.

Akizingumza na wananchi hao, Waziri Mkuu aliwataka wakazi hao wahakikishe wanaulinda huo ili uendelee kuwapa uhakika wa upatikanaji wa maji wakati wote pamoja na kuendelea kuvitunza vyanzo vyote vya maji.

Akiongea na wakazi wa Himo, Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Mheshimiwa Samia amedhamiria kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao “vijana nawapa tahadhari ukijulikana umempa mtoto wa kike mimba, sheria kali zitachukuliwa dhidi yako”


Pia aliwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ipo makini na itaendelea kuwatumikia hivyo kila mwananchi katika nafasi yake afanye kazi kwa bidii ili waweze kujiletea maendeleo.


 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU