Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameitaka taasisi ya SHELTER AFRIQUE kuratibu maonesho ya kimataifa ya dunia ya Teknolojia na ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu nchini Tanzania.

Waziri Lukuvi alitoa kauli hiyo leo tarehe 3 Septemba 2021 alipokutana na ujumbe wa taasisi hiyo katika ofisi za wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma uliokwenda kwa ajili ya kuelezea mikakati yake kwa ajili ya kutangaza mikakati yake katika kusaidia ujenzi na teknolojia rahisi ya ujenzi kwa nchi wanachama.

Lukuvi alisema, serikali iko tayari kutoa eneo kwa ajili ya kufanyika maonesho hayo kwa kushirikisha makampuni mbalimbali Duniani aliyoyaeleza kuwa yataisaidia kutangazwa kwa teknolojia za ujenzi wa nyumba bora na za gharama nafuu na hivyo kusaidia wananchi na makampuni yanayofanya kazi za ujenzi.

‘’Tunataka Shelter Afrique mratibu maonesho na wadau wengine duniani kwa ajili ya kuonesha teknolojia mpya au teknolojia nyingine kwa ajili ya ujenzi wa nyumba bora na  gharama nafuu na maonesho hayo yawe ya kidunia’’ alisema Lukuvi.

Shelter Afrique ni Taasisi ya kifedha yenye nchi wanachama 44 Barani Afrika inayosaidia maendeleo ya ujenzi kwenye sekta ya nyumba  na maendeleo ya mijini nchini Afrika ambapo hutoa bidhaa na mikopo ya fedha kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba bora za makazi kwa gharama nafuu.

Alisema, serikali iko tayari kutoa eneo la ekari hamsini kwa ajili ya kufanyika maonesho hayo kila mwaka kubainisha kuwa maonesho hayo yahusishe teknolojia rahisi ya ujenzi wa nyumba bora na vifaa vya ujenzi kwa lengo la kutoa elimu kwa makampuni ya ujenzi na wananchi kuweza kumudu gharama za ujenzi.

Kwa Tanzania Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekuwa katika jitihada kubwa za kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya kuuza na kupangisha ambapo kwa sasa Shirika hilo linaendesha miradi yake maeneo ya Iyumbu na Chamwino mkoani Dodoma.

‘’NHC kwa ina kiwanda cha kutengeneza matofali, eneo kwa ajili ya kuchimba kokoto na pia tunajenga kiwanda kwa ajili ya kutengeneza zege na tuko mbioni kuwa na kiwanda cha mabati na tutaanza kwa kazi za ndani za shirika’’ alisema Mkurugenzi wa Ujenzi wa NHC Mhandisi Hekamen Mlekio.

Waziri Lukuvi ameihakikishia taasisi ya Shelter Afrique kuwa yuko tayari kuishawishi serikali kutekeleza miradi yake kupitia teknolojia itakayotangazwa au kuonesha kuwa ni bora na ya gharama nafuu.

Kwa mujibu wa Lukuvi, serikali ya tanzania iko tayari pia kutoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji kwenye sekta ya ujenzi wa nyumba na kusissitiza kuwa bado Tanzania inayo ardhi kubwa kwa ajili ya uwekezaji.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Shelter Afrique Andrew Chimphondah ameishukuru wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ushirikiano mkubwa inaounesha kwa taasisi hiyo ikiwemo kutoa michango yake na kueleza kuwa, uamuzi wa kukutana na nchi wanachama kama Tanzania ni jitihada za kutekeleza azimio la Younde (Younde Declaration).

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo aliishiriku taasisi ya Shelter Afrique kwa kuelezea mikakato yake kwa wizara hiyo na kueleza kuwa ana imani ushirikiano baina ya wizara na taasisi hiyo utakuja matokeo chanya katika masuala ya ujenzxi wa makazi bora.