Watu wanane wameuawa kwa kupigwa risasi kwenye mji wa Perm nchini Urusi. Shambulizi hilo lililowajeruhi takriban watu wengine 20 limetokea baada ya mwanafunzi mmoja wa kiume kufyatua risasi katika Chuo Kikuu cha Perm.
Kamati ya Upelelezi ya Urusi, ambayo inachunguza matukio makubwa ya kihalifu imesema mshambuliaji huyo ameuawa.
Wakati huo huo, Chama tawala nchini Urusi cha United Russia, kinachomuunga mkono Rais Vladmir Putin, kimeendelea kuhodhi nafasi yake baada ya kushinda wingi wa viti bungeni kwenye uchaguzi.
Tume ya uchaguzi ya Urusi imetangaza leo kuwa huku nusu ya kura zikiwa zimehesabiwa katika uchaguzi huo wa bunge, chama hicho kimepata asilimia 45.9 ya kura.
Kulingana na takwimu za muda za tume ya uchaguzi, chama cha Kikomunisti kinatarajiwa kushinda kwa asilimia 21.5, chama cha kizalendo kinachofuata siasa za mrengo wa kulia cha LDPR kinatabiriwa kushinda kwa asilimia 8.1.