Na Mwandishi Wetu, Bukoba
Timu ya wataalamu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekutana na kujadiLi utekelzaji wa mradi wa kufua umeme wa Murongo/Kikagati uliopo katika mto Kagera mpakani mwa Tanzania na Uganda.

Mkutano wa Kitaifa wa Makatibu Wakuu ngazi ya Wataalamu kuhusu mradi wa kufua umeme wa Murongo/Kikagati umefanyika Mjini Bukoba kuanzia tarehe 28 – 30 Septemba, 2021 ambapo pamoja na mambo mngine, wataalamu wamepata fursa ya kujadili mambo mbalimbali kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Inategemewa kuwa mara baada ya kukamilika kwa mradi huo, utazalisha megawatts 14, na kila nchi itapata megawatts saba. Aidha, Mkutano wa Kitaifa wa Mkatibu Wakuu kwa ngazi ya Wataalamu, utafuatiwa na Mkutano wa Makatibu Wakuu utakaofanyika tarehe 01 Oktoba 2021.

Akiongelea kuhusu Mkutano wa Kitaifa wa Mkatibu Wakuu Ngazi ya Wataalamu, Kaimu Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Kijamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota amesema lengo la Mkutano huu ni kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni mafanikio na changamoto zinazo ukabili mradi kwa sasa. Aidha, Mkutano wa ngazi ya Wataalamu ni utekelezaji wa maagizo ya Mkutano wa 13 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Nishati la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwezi Novemba 2018.

Ujenzi wa Mradi huo ni makubaliano ya nchi mbili za Tanzania na Uganda ya matumizi bora ya maji ya mto Kagera ambao upo mpakani mwa nchi hizo. Mradi huo unatekelezwa/kujengwa na Kampuni binafsi ya Kikagati Power Company Limited (KPCL).

Awali ujenzi wa mradi huo wenye gharama ya dola milioni 95 ulianza Mei 2018 na sasa unatarajiwa kukamilika Oktoba 2021.