Na Dorina G. Makaya & Janeth Mesomapya
Waziri wa Nishati, Mh. January Yusuf Makamba, amewaagiza wataalamu wa Wizara ya Nishati kuunda timu itakayojumuisha sekretarieti za mikoa minane ambapo utapita mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ili kutengeneza maelezo mahususi ya mikoa hiyo yatakayofanikisha unufaikaji wa fursa zitokanazo na utekelezaji wa mradi huo.
Waziri Makamba ameyasema hayo Septemba 28, 2021 katika siku ya pili ya semina kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa mikoa hiyo inayoendelea jijini Tanga. Semina hiyo ina lengo la kubainisha fursa zitokanazo na mradi huo wa bomba la mafuta.
Ameelekeza kuwa maelezo hayo mahususi yatoe taarifa kamili kuhusu mahitaji kwenye mikoa hiyo katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi, maandalizi wanayotakiwa kuyafanya ili kukidhi mahitaji husika, thamani ya kazi kiuchumi, na mchanganuo wa fursa zitakazopatikana kulingana na mikoa hiyo na jiografia zake.
“Baada ya kupatikana maelezo hayo, iangaliwe namna bora ya kuwajengea uwezo wananchi wa mikoa husika ili wawe na uwezo wa kufanya kazi na kunufaika na fursa hizo, lengo likiwa kuwapa taarifa sahihi juu ya fursa za mradi ili wawe na mategemeo halisia” aliongeza.
Aidha, Waziri Makamba amewaagiza wasimamizi wa mradi huo, kuhakikisha Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unalenga kunufaisha jamii zinazozunguka mradi ili manufaa halisi yaonekane pindi mradi unapofikia ukomo.
Kwa upande wa kanzidata maalumu ya watoa huduma inayoendeshwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Waziri Makamba ameagiza kuwa, ufahamu wa kutosha utolewe kwa wananchi wa jinsi ya kujisajili kwenye kanzidata hiyo, ili watoa huduma wengi zaidi wawe sehemu ya jukwaa hilo.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato ameeleza kuwa, ili fursa za mradi huu zinufaishe kwanza jamii zinazopitiwa na bomba, serikali inaandaa mikakati ya kuhakikisha fursa hizo zinabaki ndani ya mikoa husika na kunufaisha watu wake.
“Tutaenda pia kwenye mikoa husika kuwaelezea wananchi fursa zilizopo kwenye mikoa yao kwa mchanganuo mzuri, ili wajiandae kuzichangamkia,” aliongeza. Naibu Waziri Byabato.
Semina hiyo ya siku tatu itamalizika leo.