Wanawake kadhaa nchini Afghanistan wameandamana mjini Kabul kudai haki ya kufanya kazi na kuhudhuria masomo katika wakati kuna ishara za kurejea kwa enzi ya sheria kali za Kiislamu chini ya utawala wa Taliban. 

Mikanda ya video iliyorushwa na vyombo kadhaa vya habari imeonesha kundi dogo la wanaharakati wakiandamana mbele ya iliyokuwa ofisi ya wizara ya masuala ya wanawake mjini Kabul wakipaza sauti kudai haki za binadamu na zile za wanawake. 

Mwanahakarakati mmoja aliyeshiriki maandamano ya leo, Fawzia Wahdat, amesema wamekusanyika kupinga kufutwa kwa wizara ya wanawake na kukosekana kwa wanawake ndani ya baraza jipya la mawaziri. 

Tangu kundi la Taliban lilipochukua udhibiti wa Afghanistan wasiwasi ni mkubwa juu ya hatma ya haki za wanawake ikitiliwa maanani kundi hilo lililaumiwa kwa ukandamizaji wa wanawake lilipoitawala nchi hiyo miaka ya 1990.