WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atapeleka timu maalumu ya wataalamu mkoani Kagera watakaofuatilia na kuhakiki mali zote za vyama vya ushirika ili kujenga mfumo bora kwenye vyama hivyo kwa manufaa ya wakulima wa Mkoa huo.
Ameyasema hayo jana (Jumatatu, Septemba 20, 2021) wakati akizungumza na wananchi baada ya kuzindua jengo la Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Kyerwa.
Amesema Serikali inataka kufahamu namna vyama hivyo vinavyojiendesha na mfumo vinaotumia katika mauzo ili kuondoa malalamiko ya wakulima kuhusu upunjwaji wa mapato.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali inataka kujua utaratibu unaotumiwa na vyama hivyo katika kuwasimamia wakulima na namna vinavyoendesha shughuli zao kwani wamiliki wa viwanda wamekuwa wakikosa mazao na vyama hivyo vimekuwa vikibeba jukumu la kununua mazao kutoka kwa wakulima jukumu ambalo lingeweza kufanywa na wamiliki wa viwanda.
Ameongeza kuwa timu hiyo itakapomaliza kufanya kazi yake itatoa mapendekezo ambayo yataiwezesha Serikali kutafanya marekebisho na kuleta tija kwa wakulima.
Waziri Mkuu alihitimisha kwa kusema Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria kusogeza huduma za kijamii karibu na tayari fedha za kutosha zimetolewa kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ya huduma za jamii.
“Mheshimiwa Rais, ana nia thabiti ya kuwahudumia Watanzania na ametoa maelekezo ambayo sisi wasaidizi wake tutahakikisha tunayasimamia na kufuatilia miradi yote inayotekelezwa kwa ubora unaostahili”.