Rais Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi aliowaapisha hii leo kwenda kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha wanaleta matokeo katika kazi wanazofanya.

Rais ametoa kauli hiyo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha Mawaziri wanne na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufuatia uteuzi alioufanya hapo jana.

Amewataka Viongozi hao kwenda kufanya madabdiliko katika maeneo yao kama kuna haja ya kufanya hivyo, na kamwe wasiogope kufanya mabadiliko yoyote yenye maslahi kwa Taifa.

Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan, mabadiliko kwa viongozi bado yanaendelea hivyo ni vema viongozi anaowateua kujituma  na kufanya kazi kwa weledi.

Amesisitiza kuwa uongozi wake utazingatia matendo makali na si maneno makali, kwani maneno makali si hulka yake.

"Nataka niwaambie, kipindi cha miezi sita nilikuwa najifunza, nilikuwa Makamu wa Rais nilikuwa na ninyi lakini sikuwa na fursa ya ndani ya kujifunza utendaji wa ndani wa Wizara hivyo nilikuwa najifunza na nimeona sasa vipi nakwenda na nyie," amesema Samia.

Amesema katika uongozi kuna mbinu nyingi na yeye amejichagulia njia yake.

"Nataka niwaambie kwamba, tunapoendelea huko, Serikali yetu itaendeshwa kwa matendo makali na siyo maneno makali. Ninaposema matendo makali siyo kupigana mijeredi ni kwenda kwa Wananchi na kutoa huduma inayotakiwa kila mtu kufanya wajibu wake.

"Msinitegemee kwa maumbile yangu haya pengine na malezi yangu kukaa hapa nianze kufoka. Nahisi si heshima, kwa sababu nafanya kazi na watu wazima wanaojua jema na baya ni lipi kwahiyo ni imani yangu kuwa tunapozungumza tunaelewana na kila mtu anajua afanye nini kwenye majukumu yake. Sitafoka kwa maneno, nitafoka kwa kalamu," amesema Samia.

Mawaziri walioapishwa katika hafla hiyo ni Dkt. Stergomena Tax kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Ashatu Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,  January Makamba kuwa Waziri wa Nishati, Profesa Makame Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Dkt. Eliezer Feleshi ambaye ameapishwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.