Kuna ishara nyingi ambazo ni vyema tukajifunza ili kuwa makini na kuchukua hatua pale unapoziona kwa mwanaume. Ni vigumu kukubaliana nazo lakini ukweli siku zote huwa unabaki palepale lazima tujifunze kama ifuatavyo:

Kutokujali

Ukiona mwanaume ameacha kabisa kukujali. Tofauti na namna ambavyo alikuwa mwanzo kwamba atakuuliza umekula, upo wapi ujue kabisa mtu huyo ameshakutoa moyoni. Kwa mtu unayempenda haiwezekani vitu hivyo vikakata ghafla na vikadumu kwa muda mrefu.

Mwanaume anakaa wiki moja, mbili na hata mwezi mzima bila kukuuliza chochote, jiongeze na uanze kuchukua hatua za kumtoa moyoni. Kama mtu hakujali ni dhahiri hana mpango na wewe, utateseka bure kuendelea kumuwaza wakati yeye anafurahia maisha ya uhusiano na mtu mwingine.

Mwanaume alikuwa akikupigia simu kila wakati, akikutumia ujumbe kila wakati lakini ghafla ameacha na anakaa muda wa mwezi au miezi bila kukupigia wala kukutumia uijumbe wowote, huyo hakutaki. Yeye hawasiliani na wewe lakini wewe kila uchwao ndiyo unakazana kumpigia.

Mbaya zaidi hata simu zako hapokei, hilo ni tatizo. Si mara moja au mara mbili unafanya hivyo lakini hajali, tambua kabisa unapoteza muda wako bure.  Mwanaume huyo anakuwa tayari ana mtu mwingine au alichokuwa anakitafuta kwako ameshakipata au pengine matarajio yake kwako sivyo alivyotegemea.

Mwingine anakuwa mtu wa kukuita pale tu anapokuwa na matamanio ya kimwili. Anakuita na baada ya hapo, hazungumzi na wewe tena. Hakupi ushirikiano wowote hadi pale atakapokuwa anahitaji kuonana na wewe ndipo anakupigia simu kwa kujifanya anakusalimia ili ukimjibu vizuri, anaomba muonane faragha.