Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imeinyoshea kidole cha lawama Urusi kuhusiana na jaribio la kutaka kuiba data kutoka kwa wabunge. 

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani, Andrea Sasse amesema nchi hiyo inashuku hayo ni maandalizi ya Urusi ya kutaka kusambaza habari za uongo kuhusu uchaguzi wa Ujerumani utakaofanyika baadae mwezi huu. 

Sasse amesema kuelekea uchaguzi huo, kumekuwa na majaribio ya kupata data binafsi za wabunge wa shirikisho na kijimbo kwa lengo la wizi. 

"Serikali ya shirikisho inachukulia jambo hili lisilokubalika kama kitisho kwa Jamhuri ya Shirikisho ya Ujerumani na mfumo wa kidemokrasia na ni mzigo kwa uhusiano wa nchi hizi mbili. 

Ujerumani inatoa wito kwa serikali ya Urusi kusitisha vitendo hivi vya mtandao mara moja."Katikati ya mwezi Julai, mkuu wa ujasusi wa ndani nchini Ujerumani alisema shirika lake liliona vitendo visivyo vya kawaida vya majaribio ya kupata taarifa kuhusu barua pepe za wabunge wa Ujerumani.