Katika kuhakikisha sekta ya utalii inaimarika na kufikia ngazi za Kimataifa Serikali ya Tanzania na Kenya zimeweka mikakati ya makubaliano ya mfumo wa kufanya kazi kwa pamoja katika kujadili na kuweka mapendekezo ya sekta hiyo
Akizungumza leo Jijini Arusha katika mkutano wa ushirikiano wa masuala ya utalii baina ya nchi hizo,Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania,Dkt.Damas Ndumbaro amesema mfumo huo utafanya kazi ya kujadili pamoja na kuweka mapendekezo mwishoni kupitishwa na Mawaziri wa sekta hiyo Kenya na Tanzania kwa ajili kusonga mbele.
"Naamini tukifanya hivyo tutaweza kutatua changamoto nyingi zinazotukabili na hatimaye kuweza kufanya sekta ya utalii ifanye vizuri zaidi kati ya nchi hizi mbili,"alisema Dkt.Ndumbaro.
Katika mkutano huo wa ushirikiano baina ya nchi mbili, Waziri wa Utalii na Wanyamapori,Mhe. Najibu Balala ameongoza ujumbe wa Kenya akiwa ameongozana na Watendaji kutoka wizara hiyo huku ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii akiwa ameambatana na Watendaji kutoka ndani na nje ya Wizara anayoiongoza.
Dkt.Ndumbaro ameongeza kuwa Sekta ya utalii ni muhimu sana kwa Kenya na Tanzania kwasababu inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi hizo mbili kwani kabla ya uviko -19 nchini Tanzania utalii na misitu ilikuwa inachangia asilimia 21.5 ya uchumi wa nchi pia ilikuwa inachangia asilimia 25 ya fedha za kigeni.
"Utalii na Misitu ilikuwa inatoa ajira takribani milioni sita kwa hiyo ni sekta muhimu kwa kuwa tunaamini kwamba bado hatujafikia pale tanapaswa kufikia na ili kuweza kufikia yatufaa tuongeze ushirikiano na majirani zetu ili tuweze kukuza utalii wetu,"alisema Waziri huyo.
Waziri Ndumbaro amesema nchi ya Kenya ni muhimu hivyo wana kila sababu ya kushirikiana nao katika kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha kwamba sekta ya utalii inaongeza tija kwani sekta hiyo ndio iliyoathirika zaidi na janga la Covid -19 hivyo serikali ya Tanzania imeendelea kutenga bajeti yake kusaidia taasisi zile zilizoshindwa kujiendesha zinapewa fedha kupitia bajeti kuu ya serikali.
"Nichukue fursa hii kuwaambia kwamba Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imepewa heshima mbili katika sekta ya utalii mwaka huu ikiwemo Tanzania kuwa mwenyeji wa kwanza wa onesho la utalii katika nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ambapo yatafanyikia hapa jijini Arusha,"amesema Waziri Ndumbaro.
Aidha Ndumbaro amesema maamuzi ya mawaziri sita nikufanya onesho hilo kuwa kubwa zaidi duniani na onyesho lingine litafanyika mwakani nchini Burundi ikiwa lengo ni kuleta wadau wote duniani waweze kutembelea nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa heshima ya pili waliipata nchini Cape Vede ambapo UNWTO iliiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa 65
Kwa upande wake Wziri wa Utalii na wanyamapori waKenya,Najibu Balala alisema nchi hizo mbili zimekubaliana kushirikiana hali ambayo itasaidia kuvuta watalii hapa nchini pamoja na nchi ya Kenya kwani ni jamii moja hata mbuga za wanyama pia zimewaunganisha.
"Naona umuhimu wa kuwa na ushirikiano upya hivyo tumekubaliana kwa miezi mitatu itakayokuja tutakuwa tumekamilisha MU na tumeunda kamati maalumu ambayo inakuwa inaongozwa na makatibu wakuu wa wizara zetu wa zetu hizi mbili na pia tumeongezea wizara nyingine ikiwemo ya uchukuzi,Teknolojia,afya,na uhamiaji nao watashiriki kwenye kamati hii,"alisema Waziri Balala.
Naibu katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki ,(EAC) Steven Mlote alisema nchi ya Tanzania na Kenya zinavivutio vingi kuliko nchi zingine ikiwa vinaingiliana mfano Serengeti na Masai Mara hivyo ni vyema wakakubaliana katika mambo ambayo yatafanya watalii wengi kuweza kutembelea nchi hizo bila vikwazo pamoja na mazungumza hayo yatachangia kuongeza utalii wa ndani.
Ikumbukwe kuwa hatua hii ya kukutana na kufanya mkutano katika ya Waziri wa Utalii wa Maliasili na Utalii wa Tanzaia na Waziri wa Utalii na Wanyamapori wa Kenya ni hatua ya utekelezaji wa kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili mara baada ya uhusiano huo kudorora kwa muda mrefu hali iliyomlazimu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassani mara tu baada ya kuapishwa kufanya ziara ya nchini Kenya ambapo alifanya mazungumzo na Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta katika kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo majirani