Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo Tanzania itapata faida nyingi za kiuchumi endapo itaridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika(AfCFTA).
Prof. Mkumbo ameyasema hayo akijumuisha maoni na mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira wakati wa semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu Mkataba huo iliyofanyika Septemba 3, 2021 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Alisema Serikali imeshafanya uchambuzi wa faida na hasara za mkataba huo na kujiridhisha kuwa faida ni kubwa kuliko hasara iwapo Tanzania itaridhia kujiunga na mkataba huo.
“ Serikali imefanya tathimini na kuona kuna faida kubwa ya kiuchumi nchi ikijiunga, na kisisani nchi yetu inajulikana kuwa mstari wa mbele kwenye ukombozi hivyo hatuwezi kurudi nyuma katika ukombozi wa kiuchumi.” Alisema Prof. Mkumbo
Akitaja faida hizo, Prof Mkumbo alitaja faida hizo kuwa ni pamoja na kupatikana kwa masoko mapya ya mazao ya kilimo na hivyo kuchochea uzalishaji wake nchini, Kuimarika kwa mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo ambayo mengi yanahusisha wakulima wadogo kama vile alizeti, pamba, karafuu, viungo, matunda na mbogamboga kutokana na kuongezeka kwa soko la bidhaa ambazo zitazalishwa nchini na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.
Faida nyingine zilizotajwa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji na ajira kwa wakulima na wadau wanahusisha katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, Upatikanaji wa bidhaa za aina mbalimbali (varieties) nchini na kupatikana kwa soko kubwa la bidhaa na huduma lenye idadi ya watu takriban bilioni 1.2 ukilinganisha na idadi ya watu takribani milioni 522 katika nchi za EAC na SADC .
Prof. Mkumbo aliendelea kufafanua faida za mkataba huo ni pamoja na kuongezeka kwa tija na ubora kwa bidhaa na huduma za Tanzania kutokana na kuongeza kwa ushindani na hivyo kupelekea kupungua kwa bei za bidhaa, sambamba na kuviendeleza Viwanda, Viwanda Vidogo na Biashara ndogo na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje ya nchi (technology transfer) kutokana na uwekezaji utakaofanyika nchini.
Aidha, Profesa alisema mkataba huo unaruhusu kutoridhia kwenye baadhi ya maeneo ambayo nchi itaona haina faida na kutolea mfano eneo ambalo Tanzania haitafungulia hususani kwenye biadhaa za nguo ili kulinda uzalishaji wa pamba unaofanyika katika mikoa 17 nchini.
Alisema mkataba huo pia umetambua utofauti wa uchumi katika nchi za Afrika na kuweka namna ya kuzisaidia nchi ambazo uchumi wake sio mzuri huku ikitoa fursa ya kujindoa baada ya miaka mitano.
Aidha, Prof. Mkumbo alitumia fursa hiyo kuwatoa hofu wabunge kuhusu kile kinachoonekana Tanzania imekuwa haifanyi vizuri katika masoko ya nje na kutolea mfano wa biashara kwa soko la Afrika Mashariki kwa mwaka 2020 ambapo mauzo ya Tanzania yalikuwa dola za Marekani milioni 812.5 ikilinganishwa na nchi hizo ambazo ziliuza bidhaa za dola za Marekani milioni 324.3 nchini.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mtangamano wa Biashara wa Wizara Bw. Ally Gugu akiwaelimisha Wajumbe hao alisema Mkataba huo unahusisha maeneo ya ushirikiano katika Itifaki ya Biashara ya Bidhaa, Huduma, Usuluhishi wa Migogoro, Uwekezaji, Haki Miliki Ubunifu, Sera za Ushindani, na Biashara Mtandao (E-Commerce).
Hivyo kuridhia mkataba huu ni muhimu kwani itaongesa wigo wa fursa nafuu za biashara na masoko ya biashara, kutoa soko la uhakika na bila kutengeneza masoko ya upendeleo na fursa zaidi ya ushindani na fursa za biashara.”
Serikali itaandaa Mkakati wa Kitaifa ambao utakuwa na Mpango Kazi wa utekelezaji utaozingatia masuala mbalimbali muhimu ili kuhakikisha Tanzania inanufaika na utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA. Baadhi ya Masuala hayo ni pamoja na utoaji elimu kwa umma, ushirikishwaji wa sekta binafsi, ujengaji uwezo wa wajasiliamali, uzalishaji unaokidhi viwango vya kimataifa, matumizi ya teknolojia na ubunifu, utafiti na uendelezaji wa miundombinu wezeshi. Alisema Bwana Gugu. ,
Mkataba huo unatoa fursa ya nchi za Afrika kuwa na nguvu ya pamoja katika kuhimili ushindani wa bidhaa zake katika soko la dunia hivyo kukuza uchumi na kuondoa umasikini miongoni mwa wananchi wake. Amesema Prof. Mkumbo.
Mkataba huo ulianzishwa baada ya Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) waliokutana katika Mkutano wa dharula mwaka 2018 na kukubalina kuridhia mkataba huo kwa lengo la kuchochea uchumi na biashara miongoni mwa nchi wanachama
Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) linahusisha nchi 55 Wanachama wa Umoja wa Afrika ambazo zina zaidi ya watu bilioni 1.2 na Pato la Taifa la jumla ya zaidi ya Dola za Kimarekani trilioni 3.4. ambapo hadi Agosti mwaka huu nchi 41 kati ya 55 zimeridhia mkataba huo na kwa Afrika Mashariki ni Tanzania na Sudan Kusini ambao hawajiridhia.