Takribani watu 3,000 wameandamana nchini Tunisia katika kupinga kile kinachoelezwa hatua ya rais nchi hiyo, Kais Saied ya Julai ya kudhibiti madaraka yote ya uongozi na kumtaka ajiuzulu.

Katika eneo, ambalo linatazamwa kitovu cha maandamano la mtaa wa Habib Bourguiba, ambayo yaliufikisha kikomo utawala wa rais wa zamani wa taifa hilo,Zine El Abidine Ben Ali, waandamanaji wamesikika wakishinikiza rais Saied ajiuzulu.

Mapema juma hili, Saied alionekana kuiweka kando katiba ya nchi hiyo ya mwaka 2014, kwa kujipa mamlaka ya kutawala kwa amri katika kipindi cha miezi miwili, baada ya mkasa mwingine wa kumfuta kazi waziri mkuu, kusimamisha shughuli za bunge na kujipa mamlaka ya utendaji.