Kuna habari zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kuandikwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari zikieleza kuwa Serikali imewataka wafanyabiashara wote wa maduka ya kubadilishia fedha za kigeni walionyang’anywa vifaa vyao na kikosi kazi kilichotumiwa na Serikali wakati wa kuifunga biashara hiyo waende kuchukua vifaa vyao.

Habari hiyo imepotosha kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb) aliyoitoa bungeni wakati akijibu swali la nyongeza namba 118 la Mbunge wa Moshi Mjini Mhe. Priscus Tarimo aliyetaka kujua hatma ya Maduka ya Kubadilishia Fedha za Kigeni, tarehe 10 Septemba, 2021.

Katika Majibu yake Mhe. Masauni alitoa kauli ya Serikali kwamba baada ya hatua zilizochukuliwa, wafanyabiashara waliitwa kufanya majadiliano na Mamlaka husika na baada ya majadiliano hayo kumalizika walitakiwa wale waliopaswa kulipa walipe na wale waliotakiwa kwenda kuchukua vifaa vyao waende wakavichukue baada ya kukamilisha taratibu.

“Nitoe wito kama kuna wafanyabiashara ambao hawajachukua vifaa vyao na wanastahili kwenda kuvichukua vifaa hivyo waende wakavichukue kwani hakuna sababu ya Serikali kukaa na mali za mtu bila sababu ya msingi” Alisema katika majibu yake
 
Taarifa inayosambazwa inapotosha kwa kueleza kuwa wafanyabiashara wote wakachukue vifaa vyao wakati kauli ya Serikali iliwataka wafanyabiashara wanaoona wanastahili kuchukua vifaa vyao wafanye hivyo baada ya kutimiza vigezo na masharti na kama kuna mapungufu yoyote basi wapeleke taarifa zao Wizara ya Fedha na Mipango ili yafanyiwe kazi.

Msimamo wa Serikali ni kwamba wafanyabiashara wa Bereau de Change waliokamilisha taratibu zinazotakiwa wakachukue vifaa na nyaraka zao. Aidha, Wizara inatoa rai kwa vyombo vya habari kutumia weledi katika kuhabarisha umma kikamilifu ili kuepusha taharuki isiyo na sababu za msingi katika jamii.

Imetolewa na:

Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO