Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali yasitisha bei mpya za mafuta zilizotangazwa hivi karibuni na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Akizungumza leo jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alisema kuwa, Serikali iliona kuna haja ya kujiridhidhisha juu ya bei hizo na kama kuna uwezekanano wa kuleta nafuu kwa wananchi.

Hivyo wakati mchakato huo ukiendelea Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alielekeza kusitishwa kwa bei mpya na kuelekeza kuendelea kwa bei za mwezi Agosti.

“Kazi inayoendelea sasa ni Kamati iliyoundwa na Mhe. Waziri Mkuu kupitia kanuni na maeneo mbalimbali yanayokusanya fedha kutoka kwenye mafuta ili kuona kama kuna namna inaweza kufanyika ili kuleta nafuu kwa wananchi” alifafanua Msemaji Mkuu wa Serikali

Aidha alisisitiza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha bei za mafuta zinakuwa nafuu kwa wananchi na hivyo kamati iliyoundwa na Mhe. Waziri Mkuu inaendelea kufanyakazi kubaini sababu zilizosababisha kupanda kwa bei za mafuta.

Katika hatua nyingine, kuhusu ugonjwa wa UVIKO-19 na chanjo, Mkurugenzi na Msemaji Mkuu wa Serikali alisema kuwa, Serikali inaendelea kukabiliana na ugonjwa huo ambapo hatua mbalimbali zinaendelea kufanyika kwa kuelemisha wananchi kuchukua tahadhari zote zilizoainishwa na Watalaamu.

“Serikali inaendelea kuwasisitiza wananchi kujitokeza kupokea chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 ambayo inatolewa nchi nzima, Wataalamu wetu wanatusisitiza kuwa chanjo ni salama na zinaokoa maisha na pia kwa wale wasiochanja ndio wanaingia katika hatari ya kuumwa sana na kupoteza maisha” alisema Msigwa

Akibainisha kuhusu zoezi la utoaji chanjo, Msigwa alisema kuwa zoezi hilo linaendelea vizuri, hadi sasa zaidi ya Watanzania 325,000 sawa na asilimia 31.5 wamepokea chanjo na hivyo Serikali inaelekeza juhudi katika kupokeleka huduma za chanjo kwa Mkoba (Outreach) yaani kuwafuata wananchi katika maeneo waliko.

Msigwa aliongeza kuwa, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, anaendelea kufanya juhudi za kupata chanjo zaidi kwa ajili ya Watanzania na yapo matumaini makubwa ya kupata chanjo baada ya shehena ya dozi 1,058,400 iliyoletwa Julai 24, 2021 kutoka Marekani kuisha.

Aidha, Serikali inawasihi wananchi waliopo katika makundi hatarishi kujitokeza kupokea chanjo hizi ili wasipate madhara ya ugonjwa mkali na vifo.