Na Immaculate Makilika – MAELEZO
 Serikali imefikia uamuzi wa kupunguza tozo za miamala ya simu kwa asilimia 30 kwa mtu anayetuma na kupokea fedha za miamala kwa viwango vyovyote vinavyotumwa na kupokea, isipokuwa wale wanaotumia kati ya shilingi sifuri hadi shilingi 999.

  Sambamba na kampuni za simu kupunguza gharama za kutuma na kupokea fedha kutoka mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine kwa asilimia 10, baada ya Serikali kujadiliana nao. Hivyo Serikali imetoa muda wa kati ya tarehe 01 Septemba hadi tarehe 07 Septemba, 2021 kwa kampuni hizo za simu kuweka sawa mitambo yao ili punguzo la asilimia 30 na asilimia 10 lianze.

 Hayo yamesemwa jana jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Habari – MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati alipokuwa akizungunza na waandishi wa habari

  Msigwa alisema “Napenda kusisitiza kuwa tozo hizi zinakusanywa kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Kama ambavyo mmejulishwa katika kipindi cha mwezi mmoja na nusu tumekusanya jumla ya shilingi bilioni 63 (hadi tarehe 31 Agosti, 2021) na sasa fedha hizi zimepelekwa katika tarafa 150 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vituo vya afya na tarafa nyingine 70 zitapelekewa fedha muda wowote kuanzia sasa kwa ajili ya kujenga Vituo vya Afya.”

 Aidha, amesema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wakakae vizuri madarasani badala ya kusoma kwenye magofu ama majengo yaliyoharibika, hivyo  fedha hizo pia zimepelekwa maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kujenga na kumaliza maboma ya vyumba vya madarasa 560 kwa ajili ya wanafunzi ambao wataanza darasa la kwanza na kidato cha kwanza mwaka 2022.

 “Mwaka ujao 2022 tunatarajia kupokea wanafunzi 933,289 ambayo ni sawa na maoteo ya  asilimia 83.7 ya wanafunzi 1,115.041 waliosajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba ikilinganishwa na wanafunzi 833,872 tuliowapokea Januari mwaka huu 2021, sasa watoto wetu hawa wanahitaji vyumba vya madarasa na madawati” alisisitiza Msigwa