Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara
Waziri wa Kilimo Prof Adolf Mkenda ametoa onyo kali kwa wanunuzi wa korosho kwa njia isiyo halali maarufu kama 'Kangomba' hali inaweza kusababisha wakulima kushindwa kuendelea kulima zao hilo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya maafisa ushirika yanayojumuisha mikoa mitano yanayofanyika mkoani mtwara amesema kuwa lazima wakemee ili kumsaidia mkulima.

Amesema kuwa serikali ina mikakati ya kuwezesha wakulima ili waendelee kulima zao hilo ambapo wanatoa pembejeo na kuwawezesha kwa namna mbalimbali ikiwemo kuimarisha ushirika na kuwawezesha maafisha ushirika na ugani ili kuwezesha zao hilo kuendelea kufanya vizuri.

“Hivi mnajua kuwa kangomba imerudi tena imerudi kwa kasi kwelikweli kwenye korosho tuwalinde wakulima kangomba inawapiga kwelikweli tusaidiane kuhimiza wakulima wasiuze kangomba tunawaacha wanaziuza hovyo hii inaua zao la korosho”

“Maafisa ushirika jiulizeni nini kinaleta kangomba je ni tamaa ya fedha au nini? Kwanini tusije na mkakati ambao utamsaidia mkulima asiuze kangomba tu aipinge na kuizuia kwa nguvu zote lakini tunamsaidiaje mkulima ili akiwa na mahitaji yenye mashiko achukue pesa kwenye AMCOS kama ilivyo kwa wafanyakazi huwezi kuendesha uchumi kwa mijeredi lakini hili jambo tusipolishikilia tutaua zao la korosho tuanze mikakati ya kujenga SACCOS ili kuwasaidia wakulima wa zao la korosho wasiuze kangomba” amesema Mkenda

Katika hatua nyingine Waziri huyo amekemea chama cha ushirika kilichopo Nanjilinji Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi kilichouza ufuta wa wakulima na kukaa na fedha za wakulima.

“Huo ni utapeli na hiyo ni jinai unawezaje kuchukua fedha za mkulima kisha ukaa nazo bila kumkabidhi mkulima lazima hatua zichukuliwe ningekuwa na uwezo ningesukuma ndani hawa kimsingi wanatuhatibia ushirika”

“Huwezi kumkopa mkulima wewe nani unazunguka na pesa ili iweje haya ni matokeo ya wakulima wachache kuwepo kwenye ushirika ambao wamekuwa wakiamua hatma ya uuzwaji wa mazao ya wakulima wengi ambao hawapo kwenye umoja huo”

“Ubadhirifu chama cha msingi Nanjilinji kilwa tutawashugulikia wamenunua ufuta kwa wakulima wanazunguka na fesha za wakulima tutawachukulia hatua, hizo fedha ni za wakulima wachache wameweka utaratibu lazima mazao yapitie kwenye ushirika” amesema Mkenda

Nae Mrajis Mkuu wa Vyama vya Ushirika nchini Dkt Benson Ndiege amesema kuwa mafunzo hayo yanajumuisha vyama zaidi ya 9000 nchini ambapo zaidi ya maofisa 400 watajengewa uwezo.

“Tunahitaji kujenga ushirika mpya nchini ili tufanye mabadiliko kwenye ushirika ili tuwe na watu wenye uwezo wa kufanya kaguzi wenyewe kabla hawajakaguliwa mfano mwaka 2019/20 ukaguzi ulifanyika chini ya asilimia 60 lakini maofisa wenye uwezo wa kujikagua walikuwa 33 lakini pia hawakujikagua ndio maana tunawajenga uwezo ili waweze kujikagua wenyewe na kuwapa vitendea kazi”

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa Queen Sendiga amesema kuwa vyama vya ushirika vimekuwa sehemu ya utendaji kazi usio na maadili ambao una fifisha jitihada za wakulima huku ubadhilifu wa fedha ukitajwa kwa kiasi kikubwa kutokea katika vyama hivyo.