WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imedhamiria kujenga vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) katika kila halmashauri nchini.

Amesema kuwa lengo la ujenzi wa vyuo hivyo ni kuhakikisha vinatoa elimu ya ujuzi maalum kwa vijana wa Kitanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo utaalam wa TEHAMA, Ufundi Umeme, makenika na maeneo mengine.

Amesema hayo jana Ijumaa (Septemba 17, 2021) wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya Buhingwe ambacho kitagharimu shilingi bilioni 2.4 mpaka kukamilika kwake, ambapo mpaka sasa kiasi cha shilingi bilioni 1.6 zimeshatumika.

“Tulianza na ujezi wa vyuo vya VETA kimoja kimoja kila mkoa, sasa tunashuka chini kwenye kila halmashauri, chuo hichi nimeweka jiwe la msingi leo, maana yake hakitasimama, kitajengwa mpaka kikamilike kwa ajili ya vijana wetu kupata eneo la kujiongezea ujuzi”

Aidha, Waziri Mkuu amepongeza VETA kwa kusimamia maelekezo ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya ujenzi wa chuo hicho ambacho kitakuwa mkombozi kwa vijana “Endeleeni kuwa na imani ya Serikali yenu”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga amesema kuwa katika awamu ya kwanza wanajenga vyuo vya VETA  29 na zitatumika zaidi ya shilingi bilioni 48.6. “Tutasimamia ujenzi wa vyuo hivi kwa weledi na umakini mkubwa ili kuhakikisha maono ya Rais Samia yanatimia”

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pacras Bujulu amesema kuwa chuo hicho ambacho kinajengwa kwa gharama za Serikali, kinatarajiwa kuanza kutoa mafunzo ifikapo mwezi Januari, 2022 na mpaka sasa majengo 15 kati ya 17 yameshaezekwa.

Akiongea na wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu baada ya kukagua shamba za chikichi linalomilikwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Msalaba Mwekundu amewataka wakazi hao kulima zao la chikichi kwa kuwa linafaida kubwa na kwa muda mrefu “chikichi hii unaweza kuivuan kwa miaka 30

Aliongeza kuwa mwaka 2018 Serikali iliamua kuanzisha mbegu yake ya Chikichi  ambayo ni bora zitakazolimwa lengo ni kuhakikisha nchi inajiongezea uchumi kupitia zao la chikichi.

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU